Yajue maajabu ya nyanya

22 Sep 2014

  Je, wajua kuwa nyanya hupunguza uwezekano wa kupata saratani?

  Nyanya ni tunda muhimu na lililozoeleka kuliko mengi. Mara nyingi huchukuliwa kama kiungo zaidi kuliko tunda Ia kuliwa lenyewe, huku likidhaniwa kuwa halina kazi ya ziada kwenye mwili zaidi ya kukifanya chakula kiwe na ladha nzuri. Lakini wataalamu wa afya wamegundua kwamba tunda hili lina uwezo mkubwa wa kupunguza uwezekano kwa mlaji asipate saratani hasa ya tezi dume na ya utumbo mkubwa!

  Dkt. Don Colbert (1999), anasema tunda hili sio tu kwamba ni zuri kula lenyewe, bali pia lina lishe-mmea (phytonutrients) aina tatu zenye uwezo wa kuzuia visababishi vya saratani (carcinogen) visiweze kuhimiza chembechembe hai za mwili zisianze kukua hovyo na kuwa saratani. Lycopene, iliyoko kwenye nyanya ina uwezo mkubwa wa kuzuia aina hizo za gonjwa hili hatari (saratani ya tezi dume na ya utumbo mkubwa). Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Health Professionals Fellowship, mwanaume anayekula milo kumi yenye nyanya kila wiki anapunguza uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume kwa45%. Hii inakuwaje? Ni kwa sababu ya jinsi saratani yenyewe inavyoanza na kukua kwenye mwili.

  Jinsi Saratani inavyoanza kwenye mwili

  IIi saratani itokee kwenye mwili kunahitajika vitu viwili: kiazilishi (initiator) na kichocheo (promoter). Mifano ya viazilishi ni tumbaku. Dkt. Colbert anasema, "Mtu anapovuta sigara, mchakato wa kuanzisha saratani kwa kweli unakuwa umeanzishwa na tumbaku. Lakini saratani hiyo haichanui mpaka kupatikane kichocheo. Hiki ni kitu chochote chenye uwezo wa kuifanya chembe-hai (cell) ianze mwendo wa kukua kinyume na mpangilio wa asili." Huku kukua hovyo kwa chembe-hai ndiyo saratani yenyewe.

  Mwanamume anaweza akawa na saratani ya tezi dume katika hatua changa sana. lakini akipewa testosterone, inaweza kuichochea ikakuwa haraka. Vichocheo vingine vya saratani ni pamoja na mafuta, au vyakula vyenye kolestero (cholesterol), na nyama nyekundu. Vyenyewe havisababishi ugonjwa huu lakini huchochea utokee.

  Kwa hiyo unapopata kwenye mwili kiini kama cha lycopene, iliyoko kwenye nyanya, inayopigana na viazilishi au vichocheo vya saratani, ni kama kuleta askari walinzi kwenye mwili wako. Kwa sababu hiyo, Dkt. Colbert anashauri, mtu mzima ale angalau nyanya mbili zisizopikwa kila siku.

  About Author

  Super User