×

Warning

JUser: :_load: Unable to load user with ID: 886

MISINGI YA UONGOZI

31 Aug 2016

  1.0 Utangulizi

  Hakuna taasisi itakayofanya kazi vizuri bila kuwa na uongozi bora. Uongozi ndio chanzo cha mafanikio yote yanayopatikana katika jamii, taasisi, kampuni, chama, au katika chombo chochote cha kiserikali, kidini au kibinafsi. Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya watu wanadhani kuwa maendeleo yanaletwa na uwingi wa raslimali, watu, sera, na sheria pekee. Lakini ukweli ni kuwa, hata kama hayo yote yakiwepo, bila kuwa na uongozi mahiri, hakutakuwa na mafanikio yoyote ya kimaandeleo, kimaadili, na kimaisha kwa taasisi au jamii hiyo. Kwa mantiki hiyo basi, ni muhimu sana kwa viongozi wote wa kuchaguliwa, kuteuliwa, au kusimikwa na mamlaka za kidini wajue dhana mzima ya uongozi pamoja na kupata ujuzi utakaoboresha utendaji kazi zao kama viongozi.

   

  Je, wewe kama kiongozi, umewahi kujiuliza maswali mazito kama yaliyoanishwa hapo chini? Kama mwandishi mmoja (David Campbell, 1980) anavyoandika, ni vizuri kiongozi akajiuliza maswali kama haya hapa chini ili aweze kujitathmini uongozi wake:

  Kama mimi ni msimamizi wa mahali hapa:

  -       kwa nini watu wananicheka au wananidharau?

  -       Kwa nini kila mmoja ana hasira au hana furaha na mimi?

  -       Kwa nini miradi yetu haifanikiwi vizuri?

  -       Kwa nini rasilimali zinapotea bure? 

  -       Kwa nini sipati ushirikiano wa kutosha?

  -       N.k

  Maswali kama haya yataanza kukufanya ufikirie kwa undani na upana juu ya uwezo wako kama kiongozi. Mwisho wa yote utaona unahitaji kujifunza zaidi juu ya uongozi. Umuhimu wa kujifunza uongozi hauna mjadala. Wao wanaodhani wanaujua uongozi, eti kwa sababu tu wamepewa kazi hiyo na wananchi, serikali au wameitwa na Mungu, wanajidanganya. Nabii Musa alidhania anafanya vizuri katika uongozi wake mpaka aliposhauriwa na Mkwewe (Jethro), kuhani wa kutoka Midiani, ambaye alikuwa haijui vizuri imani ya Nabii Musa na Mungu wake (Kutoka 18: 13-24).

  2.0 Umuhimu wa Kujifunza Uongozi

  Upo umuhimu mkubwa sana wa kujifunza uongozi kwa sababu binadamu yeyote kwa asili hajui ambacho hajui. Ukweli ni kwamba tunajua tu kile kidogo ambacho tunajua, lakini kuna mambo mengi mno ambayo hatujui. Kwa hiyo, si rahisi kujitathmini kile ambacho hatujui. Kwa sababu ya kutojua vizuri dhana ya uongozi na stadi zake, viongozi wengi wameghubikwa na dhana potofu kama hizi zifuatazo:

  ·      Kudhania wanajua kila kitu eti kwa sababu tu wao wamepewa cheo fulani cha kuongoza wengine.

  ·      Kudhania wao ni waamuzi wa kila kitu kwa niaba ya wengine, hata kama watu wanataka kushirikishwa kwenye maamuzi hayo.

  ·      Kudhania kuwa wao hawahojiwi kitu chochote eti kwa sababu wanataka kuheshimiwa sana kushinda wale wanaoongozwa.

  ·      Kudhania kuwa matakwa yao ni ya maana zaidi kuliko matakwa ya wale wanaowatumikia.

  ·      Kudhania kuwa kujadiliana na watu na kufikia muafaka kwa pamoja ni dalili ya udhaifu.

  ·      Kudhania kuwa kutumia nguvu na vitisho ni dalili ya umahiri wa kiongozi katika jamii.

  ·      Kudhania kuwa viongozi hawakosei kwa sababu wana cheo. Na kama wakikosea, basi makosa yao yanasameheka tu kirahisi hata kama madhara yake kwa jamii ni makubwa.

  Dhana hizi na nyinginezo nyingi zenye upotofu zinadhihirisha jinsi ambavyo viongozi na wale wote wanaopenda kuwa viongozi wanavyohitaji kupata elimu na ujuzi wa uongozi. Makala haya  yanakusudia kuonyesha mambo machache ya msingi ambayo kiongozi anapaswa kuyajua. Hata hivyo, mafunzo ya uongozi ni mapana zaidi ya yale yaliyoelezwa ndani ya makala haya; kwa hiyo, litakuwa ni mwanzo wa mfululizo wa makala mengi ya kuwajengea uwezo viongozi. Wapendao kuwa viongozi na wale walioingia kwenye huduma hiyo, wanashauriwa kutumia kila fursa inayopatikana ya kujifunza uongozi.

  Ukweli ni kuwa, ukipata mafunzo bora ya uongozi; picha yako ya uongozi, utendaji wako kama kiongozi, na mwitikio wa wafuasi wako vitabadilika kabisa. Utakuwa kiongozi mwenye mafanikio makubwa. Kwa hiyo, viongozi wanahitaji mafunzo ili, pamoja na mambo mengine, waweze: (1) kuelewa dhana na nadharia ya uongozi kwa undani na upana, (3) kupata stadi za uongozi, (3) kuelewa namna ya kutenda kama kiongozi, (4) wapate kuwa na maadili ya uongozi, (5) waweze kujua namna ya kuwapa watu wao huduma iliyotukuka.

  3.0 Umuhimu na Maana ya Uongozi

  Ili tuweze kujifunza vizuri dhana ya uongozi na stadi zake, ni vizuri tukaelewa kwanza umuhimu na maana ya uongozi. Kwa kiasi kikubwa, maana ya uongozi imekuwa kitendawili kwa baadhi ya watu. Wengine wamedhania kuwa uongozi ni kile cheo anachopewa mtu anapopata kazi ile ya uongozi. Ukweli uongozi siyo jina la cheo apatacho mtu; uongozi ni kitu kikubwa zaidi.

   

  3.1 Kwa nini Uongozi?

  Uongozi ni kitu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Ni ufunguo wa mafanikio yote yanayohitajika kwenye taasisi au jamii husika. Bila uongozi bora, jamii au taasisi husika itapata shida nyingi kama zifuatazo:

  -       Vitu vya maendeleo havitatokea katika taasisi

  -       Hakuna uboreshwaji utakaotokea katika taasisi

  -       Hakuna tofauti ya kiutendaji itakayoonekana katika taasisi

  -       Kazi mbalimbali hazitasimamiwa vizuri na matukio mbalimbali hayataratibiwa

  -       Rasilimali hazitatumika vyema na  malengo hayatafanikiwa

  -       Watu hawatahamasishwa kufanya vitu vikubwa na vya kipekee

  -       Kikundi hakiwezi kufanya kama timu ya ushindi

  -       Mwisho wa yote taasisi inaweza kupoteza mwelekeo

   

  3.2 Uongozi ni Nini?

  Tafsiri rahisi ya uongozi ni: Uwezo wa mtu kuhamasisha wengine au kikundi ili kufikia malengo. Ili kuelewa vizuri maana ya dhana pana ya uongozi, tunaweza kufafanua maana ya uongozi kwa kutumia vigezo kadhaa kama ilivyoelezwa hapa chini. Vigezo vitano amevitumia Campbell (1980) kufafanua dhana ya uongozi kama ifuatavyo:

  ·      Kwa kigezo cha matokeo, uongozi ni:

  o   Kufanya vitu vitokee

  o   Kuleta tofauti chanya kwenye jamii/taasisi

  o   kusababisha malengo kufikiwa

  ·      Kwa kigezo cha mchakato, uongozi ni:

  o   Kuwezesha mfululizo wa vitendo vyenye tija

  o   Kuhamasisha watu watende kazi

  o   Kuliwezesha kundi kufanya kazi kama timu

  ·      Kwa kigezo cha vitendo, uongozi ni:

  o   Kitendo chochote kinachokusanya na kuratibu matumizi ya rasilimali ili kutengeneza fursa mpya kwa watu wanaongozwa. Rasilimali zinazoratibiwa na kiongozi ni – muda, nishati, watu, fedha, vipaji, maoni ya umma, taratibu za sheria n.k. Fursa mpya ambazo kiongozi anatakiwa kuzitafuta ni pamoja na  ajira mpya, mawazo ya biashara, faida kubwa, huduma bora, burudani bora, safari, furaha, elimu, upendo, utajiri, maisha marefu, n.k.

  o   Uongozi ni utendaji uliochangamka – kiakili, kisaikolojia, na kijamii - kwa kuhusisha wengine. Uongozi sio kuzubaa au kuwa mtu wa kusukumwa sukumwa na watu kiutendaji.

  ·      Kwa kigezo cha tabia, uongozi ni:

  o   Tabia ya kujenga mahusiano na watu

  o   Tabia ya kufuatilia majukumu

  o   Tabia ya kujisadakisha kwa ajili ya watu

  o   Uwezo wa kuchanganya tabia ya kupenda majukumu na tabia ya mahusiano (kutegemeana na hali halisi ya watu na taasisi yao).

  ·      Kwa kigezo cha tuzo la ndani: uongozi ni:

  o   Kitu kiletacho faraja baada ya kufanikisha malengo

  o   Kitu kiletacho deni kama  hujafanikisha malengo

  Kwa ufupi, uongozi sio cheo mtu alicho nacho, na wala si ubabe au nguvu alizo nazo mtu. Bali, ni uwezo wa kugusa maisha ya watu, kuonyesha tabia ya mahusiano, kujisadakisha, kusababisha mabadiliko/maboresho, na kujali mafanikio ya watu wako. Kama vile chupa ya soda inavyokuwa na nembo yenye jina la kinywaji, vilevile mtu anabeba jina la cheo. Lakini ukweli ni kwamba, kama vile ilivyo kwa soda – soda ni kile kilichomo ndani ya chupa, sio maandishi yaliyoko kwenye chupa. Hivyo hivyo na uongozi wa mtu uko ndani yake na si kwenye jina au nembo aliyoibeba nje; yaani jina la cheo chake.

  Author: Dr. Peter Mateso

   

  About Author