uongozi unakuzwa ama sivyo unadumaa...

11 Aug 2016

   

  Kwenye uwanja huu wa uongozi, Mwalimu Dkt. Peter Mateso amekuwa akipakua mengi yahusuyo uongozi. Hebu tuangalie mambo muhimu kiongozi anatakiwa kuwa makini nayo katika kupata kile kiitwacho "UONGOZI BORA"

  Maarifa

  Katika eneo la maarifa, kiongozi anatakiwa kujifunza nadharia na dhana mbalimbali za uongozi. Ni kweli kuwa taaluma ya uongozi haijaanza kutafitiwa miaka mingi kama taaluma zingine za sheria, madawa, kilimo n.k. Hata hivyo, kuanzia karne ya 20 tafiti nyingi zimefanyika na maarifa mengi yameanza kukusanywa na kufundishwa katika vyuo vingi duniani.

  Mafunzo ya Uongozi (Leadership Studies) ni moja ya taaluma inayokua na kupendwa na watu wengi wanaotaka kuongoza wengine. Zipo nadharia karibu 13 ambazo zinafahamika na zimeandikwa na watafiti/waandishi mbalimbali. Katika matoleo yajayo tutapata fursa ya kuangalia nadharia kadhaa ili wasomaji wapate picha ya baadhi ya maarifa kiongozi anahitajika kujifunza.

  Tabia (Attitude)

  Mbali na stadi na maarifa, kuna jambo la msingi sana ambalo taaluma yeyote haitafanya vizuri na wateja hawataridhika kama litakosekana. Jambo hilo linaitwa tabia (attitude). Tabia ni namna mtu anavyofanya kazi na kuhusika na wengine.

  Tabia mbaya huharibu kazi njema za mtaalamu yeyote yule. Daktari, mwalimu, au mwanasheria aliye na tabia mbaya hawezi kufanya kazi inayokubalika na wateja wake. Kiongozi naye, anatakiwa kuwa na tabia njema. Zipo tabia zinazochochea mafanikio na zipo tabia zinazochochea uharibifu, hata kama uharibifu huo hauji moja kwa moja. Kwa mfano, tabia ya kudharau wateja au wafuasi wako haiwezi kuleta mafanikio mazuri ya kiuongozi. Tabia ya kutosikiliza vizuri wafuasi wako, haiwezi kujenga mahusiano mazuri na watu wako ambao wanahitajika kufanikisha malengo ya taasisi. Mifano ya tabia haribifu iko mingi – ubabe, ubinafsi, ujeuri, kiburi, majigambo, unyanyasaji, n.k.

  Watu wengi hawajifunzi uongozi wala kutilia maanani dhana ya kujiendeleza wenyewe kwa sababu hawajui kuwa hawajui. Yule anayejitambua kuwa ana uhitaji wa kuongeza ujuzi ni rahisi kujifunza na kufurahia mafunzo yake. Bali mtu ambaye hajui ambacho hajui hawezi kujifunza lolote. Watu wasiojua kuwa hawajui au wasiokubali kuwa wana mapungufu ya kujazia wanaweza kuwa chanzo cha shida katika jamii au taasisi kama wakipata nafasi nyeti za uongozi, isipokuwa tu wamesaidiwa kufahamu kuwa hawajui kila kitu ili wafundishike.

  Uongozi ni kitu kigumu (complex), kwani una sura nyingi sana. Kwa hiyo ni muhimu kila anayejidhania kuwa anaongoza watu ajifunze taaluma hiyo. Kipaji cha kuzaliwa peke yake hakitoshi. Tunahitaji kujifunza uongozi ili tufanye vizuri zaidi na kukua katika uongozi. Hakuna njia mbadala, wote wanaopenda au wanaofanya kazi ya uongozi lazima wakue kwa kujifunza kila siku.

  Kuna njia nyingi za kujifunza. Tunajifunza kwa kusoma vitabu mbalimbali, majarida na hata mada kutoka magazetini. Aidha, tunajifunza kutoka kwa watu wengine - kama vile wafuasi wetu, waalimu, marafiki, na viongozi wenzetu au waliotutangulia. Pia, tunajifunza kutokana na makosa yetu wenyewe na ya wengine.

  Zaidi ya yote, vipo vyuo au taasisi zinazotoa mafunzo ya uongozi sehemu mbalimbali duniani. Usikubali kuambiwa kuwa uongozi hauna shule. Kujifunza ni mchakato wa kila siku. Nia ni kufanya vizuri zaidi. Ukitaka kufanikiwa kesho, jifunze leo. Ukisubiri kesho hiyohiyo utakuwa umechelewa.

  Usipokubali kukuza uongozi wako kwa kujifunza, si kwamba utaudumaza tu, bali pia unajiweka katika nafasi ya kuwaletea watu wako na taasisi yako madhara yatakayotokana na makosa ambayo yangeweza kuepukwa. Kumbuka kuwa cheo cha mtu hakipungui kwa mtu kukubali kufundishika.

  About Author

  Freedom Richard