Tahadhari: matunda na mbogamboga nyingine zina sumu!

19 Jul 2016

  Matunda na mboga ni sehemu muhimu sana ya chakula. Kwa kweli hatuwi kusema tunakula mlo kamili wenye uwiano ikiwa hatutumii matunda na mboga za majani. Lakini pia vitu hivi ndiyo vilivyo na hatari kubwa ya kutuua kwa sumu ya madawa.

  Moja ya mambo yanayopigiwa kelele na mataalamu wa afya ni hatari ya kujikuta unakula sumu ya kuua wadudu (pesticides) kwa kula baadhi ya matunda na mboga za majani. Sote tunajua jinsi mboga kama mchicha, mnafu, spinach zinavyotumiwa kwa wingi mijini na vijijini.

  Karibu kila mtaa mijini utasikia miito ya kibiashara ikiwaalika walaji kununua mchicha, majani ya maboga, matembele, mchicha nk. Bahati mbaya sana hakuna mtu anayeuliza kama hizo mboga zilipuliziwa dawa ya kuua wadudu zilipokuwa zikikuzwa au la. Mbaya zaidi baadhi yake huwa zina siku chache tu tangu kupata dawa hizo ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.

  Kuna haja ya kufanya utafiti ili kuona ni kiasi gani cha maradhi na vifo vinavyotokana na ulaji wa matunda na mboga zenye sumu nchini. Lakini kwamba madhara hayo yapo haikanushiki hata kidogo. Wataalamu wa afya wanashauri kwamba walaji wawe na umakini wa ziada katika matumizi ya baadhi ya aina ya matunda na mboga za majani.

  Dr. Don Colbert (1999) anashauri; “unapofikiri ule matunda gani, zingatia yafuatayo: kama ganda la tunda ni nene basi ujue ni salama kwa kuliwa. Kwa mfano ndizi zina sumu sifuri. Ndizi ni moja ya matunda bora unayoweza kula. Machungwa, malimau, mananasi, tikiti maji na tini nayo ni mazuri sana.”

  Akizungumzia aina ya matunda yaliyo hatari kuliwa Dkt. Colbert anaonya kwamba yale yenye ganda la nje laini au jembamba ndiyo hatari sana. matunda haya ni kama Apple, pears, grapes, peaches, zabibu. Inashauriwa ule yale yaliooteshwa na kukuzwa bila kupuliziwa dawa. Na kama ni ukiyakosa yaoshe sana kwa maji yatiririkayo.

  About Author

  Super User