Hofu, Shimo, na Mtego Vinakuja

Moja ya mipaka tuliyo nayo wanadamu ni kutofahamu kwa uhakika yatakayojiri wakati ujao. Jinsi gani wataalamu wa mipango wanatamani kama wangeweza kuchungulia mbele ili waweze kupanga mambo ya miaka ijayo leo! Mtu anapokwenda stendi ya mabasi ili kusafiri, angelijua kama basi analopanda litapata ajali itakayomuua au kumfanya kilema asingelipanda. Bwana au bibi arusi angemwacha mchumba wake mara moja hata kama anampenda kama moyo wake mwenyewe, kama tu angeweza kuona mbele katika safari ya ndoa yao na kugundua kwamba mwenzake atageuka kuwa muuaji wake siku moja; lakini kama wahenga wasemavyo, majuto ni mjukuu, mwisho huja kinyume.

Je, Muumba wa wanadamu amewaacha gizani kabisa watu wake hata mambo makubwa yawapate kama mtego unasavyo bila tahadhari yoyote? Je inawezekana dunia kujua yaliyo mbele yake na kujiandaa nayo? Kila siku kuna watu wanaoiacha dunia hii na kuelekea kwenye ulimwengu wa umilele wakiwa hawakujiandaa hata kidogo na hali hiyo, je ndio mpango wa Mungu kwao huo, au kuna uwezekano wa kujua yajayo na kujiweka tayari?

Pengine kubwa zaidi tujiulize, hali ya dunia huko tuendako itakuwaje? Je, kuna uwezekano wa kuchungulia mbele na kujua yanayotujilia wanadamu kesho ili tujiandae kuyapokea au kuyaepuka? Hili ndilo ninalotaka tulitazame leo hapa; yaani yale tuliyoambiwa bayana kwamba yatautokea ulimwengu wetu siku za mwisho, na jinsi hayo yalivyokaribia sana siku zetu hizi tulizo nazo sasa.

Dunia ina historia ya kupigwa na Muumba wake kwa viwango tofauti katika vizazi vilivyopita. Lakini kabla ya mapigo ya hukumu ya Mungu kushuka juu yao daima huwa kuna sauti ya maonyo inayowafikia. Tatizo huwa ni kupuuza maonyo hayo na kwa kutokuyaamini, sio kutokujua yajayo. Ufahamu wa kidunia (secular mind) usiokubaliana na mambo ya rohoni huwazuia kupata ufunuo wa Neno la unabii juu yao, kwa sababu kwake mambo hayo huonekana kama upuuzi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa kizazi cha Nuhu, na hata wakati wa kuhukumiwa kwa Sodoma na Gomora (Mwa 6:13-7:24, 19:1-29). Dunia yetu ya sasa inakabiliwa na majanga makubwa kuliko yale ya siku za Nuhu na Lutu wa Sodoma; lakini kama ilivyokuwa kwa wale wa kale, watu wa leo nao hawana nafasi mioyoni mwao kusikia maonyo ya Neno la unabii. Wanadhani mambo yatakwenda kama walivyozoea siku zote na mtu akiwaambia yaliyo mbele yao huwa wabishi, wala hawajifunzi kutokana na historia. Neno la Unabii ndilo Dira ya Wanadamu

Muumba wetu hakutuacha gizani kamwe kwa habari ya yale yajayo. Kwa watu wa Mungu ule mpaka wa kutokujua yajayo ni mwembamba sana. Kwa kweli hakuna jambo muhimu lolote lipaswalo kumpata mtu wa Mungu kabla ya kupata taarifa yake toka kwa Bwana. Na hatima ya dunia nayo pia kwa mcha Mungu sio fumbo hata kidogo kama wengi wanavyofikiri. Yale yajayo yanajulikana kwao kama waijuavyo jana iliyokwisha kupita! Roho Mtakatifu anasema; “Siri ya Bwana iko kwao wamchao, naye atawajulisha agano lake” (Zab 25:14).

Kuna watu wanadhani haiwezekani kujua ajapo Bwana na yale yatakayoambatana na kuja kwake. Ijapokuwa kweli hatuwezi kujua siku wala mwezi wala mwaka wa, twaweza kabisa kujua majira ya ujio wake na mambo gani dunia itarajie kipindi hicho. Ikumbukwe kwamba hata alipokuja kwa mara kwanza kama Mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu kuna wachache waliofahamu. Kama tulivyoona hapo juu; “siri ya Bwana iko kwa wamchao.” Wale waliokuwa wakimcha Mungu siku zile walijulishwa siri ya ujio wa Masihi wao. Baadhi ya hawa ni Wachungaji wa makondeni, mamajusi wa mashariki, Simeoni na nabii Ana hekaluni (Luka 2:8-38, Math 2:1-12).

Roho Mtakatifu alikwisha sema zamani kwamba; “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake” (Amos 3:7). Suala la ujio wa Yesu mara ya pili ni kubwa sana, Bwana asingeweza kutuacha gizani kwa jambo kuu kama hili. Kwa hiyo aliwajulisha watumishi wake manabii mambo yote yanayohusiana na siku za mwisho na kuja kwa Kristo, akawaamuru wayaandike kwa faida ya wacha Mungu wake wa siku zetu.

Pamoja na hayo ametupa Roho Mtakatifu anayetufunulia yale aliyowaamuru manabii watuandikie. Akatupa na alama na dalili za nyakati ili tutakapoziona kwa msaada wake tujue kwamba yale yaliyoandikwa zamani yamefikia wakati wake wa kutimizwa. Maandiko hayo ndiyo lile aliloliita Mtume Petro “Neno la unabii” tulilopewa kama “taa ing’aayo mahali penye giza” (2Petr 1:19). Hii ndiyo maana tunasema hatukuachwa gizani kwa habari ya siku za mwisho; tunalo Neno la unabii.

Neno hili ni dira ya Mcha Mungu katika safari yake ndefu kwenye bahari kuu ya maisha. Mmoja wa manabii waliotuchorea ramani hii ni Isaya. Yeye alituambia kwamba siku za mwisho, dunia itakabiliwa na majanga anayoyataja kwa maneno matatu: Hofu, shimo, na mtego. Ni nini vitu hivi? Hebu tuviangalie kwa karibu hapa chini. Hofu, Shimo, na Mtego

Nabii huyu ni miongoni mwa watumishi waliotumiwa na Bwana kuandika kwa kina mambo yamhusuyo Masihi aliye Mwokozi wa ulimwengu. Anaitwa kwa haki “nabii wa wokovu” kwa sababu aliandika mambo ya wokovu wetu kana kwamba ni mtumishi aliyeishi siku za Agano jipya. Alitabiri kuzaliwa kwa Kriso (7:14), maisha na huduma yake (11:1-3), kufa na kufufuka kwake (53:4-12), kuwafufua watu wake waliokufa na kulinyakua kanisa (26:19-20), kuipiga kwake dunia katika kile kipindi kijulikanacho kama “dhiki kuu” (26:21-27:1), na kurudi tena duniani kutawala miaka elfu (2:2-4, 24:23); na hayo ni maandiko machache tu kati ya mengi aliyotupa.

Alipozungumzia kuja kwake kutawala dunia alitabiri mashaka makubwa yatakayowapata wanadamu miaka michache kabla tu ya ujio huo na ufalme wake wa amani duniani. Aliyaweka majanga hayo katika maneno matatu: hofu, shimo, na mtego. Kama asimamaye juu ya dunia akiangalia yanayoinyemelea bila yenyewe kujua, Nabii huyu alisema: Isaya 24:17-23

17Hofu na shimo na mtego vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. 18Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. 19Dunia kuvunjika inavunjika sana; 20dunia kupasuka imepasuka sana, dunia kutikisika imetikisika sana. dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela, na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka wala haitainuka tena.

21Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; 22nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa. 23Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele za wazee wake kwa ufukufu.

Huu ni unabii mzito sana; hakuna mwenye akili awezaye ku-upuuza hata kidogo. Uzito wake unaonekana kwenye ule ukweli kwamba unataja bayana hatima ya dunia kwa maana ya mfumo uliopo sasa. Unatuambia “itaanguka na wala haitainuka tena” (ms. 20)! Hapa Roho Mtakatifu aonaye wakati ujao anaainisha matukio yanayotarajiwa kuikumba dunia kuelekea mwisho wa dahari, utakaosimika kipindi kipya duniani ambapo “BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu , na mbele ya wazee wake kwa utukufu” (ms. 23).

Iko dhahiri hapa kwamba huku “kutawala…kwa utukufu” kutakuwa ndio kile kipindi kijulikanacho kama “utawala wa Kristo wa miaka elfu” (Ufu 20:6). Na hiki kipindi kitakuja baada ya mfumo wa sasa kuanguka kama alivyotabiri nabii Danieli na Mtume Yohana. Nabii huyu anatuambia hapa kwamba sababu ya mfumo wa dunia hii kuanguka ni kule kulemewa na dhambi zake. Kabla ya kuanguka, anasema; wanadamu watashuhudia dunia yao “ikivunjika sana, na kupasuka sana, na kutikisika sana, huku ikilewa-lewa kama mlevi na kuwaya-waya kama machela katika kulemewa na dhambi zake” (ms.19-20).

Katika hali hiyo, ndipo majanga matatu haya: hofu, shimo, na mtego, yatakapokuwa yanawafika wanadamu. Hofu hapa ni utisho utakaoletwa na matazamio ya mapigo yasiyozuilika ya “njaa, tauni (maradhi makubwa ya siku za mwisho yasiyo na tiba), vita kila mahali, na majanga ya asili kama matetemeko makubwa, mafuriko makubwa, vimbunga na sunami kali” (Luk 21:10-11, 25-28). Shimo ni kule waangukiapo wale wakimbiao sauti ya hofu. Wako watakaodhani ili kukomesha chokochoko inayoletwa na taifa moja ni muhimu kulipiga kijeshi kumbe wanaamsha vita visivyokoma na maangamizi makubwa.

Hakuna kitakachoshikika siku za mwisho, kila mpango wa suluhu utakuwa “shimo” la kutumbukia wanaojaribu kuikimbia “sauti ya hofu.” Lakini pia mtu akifanikiwa kutoka kwenye hali au shimo hilo atakutana na “mtego,” yaani kile kinachomkamata na kumtia mikononi mwa adui yake. Dunia inakaribia kuingia kwenye mtego mkubwa kuliko yote, wa kumkubali mtawala mbaya kabisa ajulikanaye kwenye unabii kama “mpinga-kristo” wakidhani ni dawa ya kutoka kwenye “shimo” la majanga ya kiuchumi, kisiasa, na kidini. Mtikisiko Umekwisha- Anza!

Tayari dunia inatikisika, inapasuka, na kuwaya-waya chini ya mzigo wake mkubwa wa dhambi zinazozidi kuongezeka kila iitwapo leo. Mmomonyoko mkubwa wa maadili, kuhalalishwa kwa machukizo ya ndoa ya jinsia moja, udhalimu wa watawala wa mataifa ya dunia, mauaji na dhuluma kila kona vimeilemea hii dunia sasa na kuiweka mahali ambapo anguko lake ni saa yoyote. Ni muhimu kufahamu kwamba kila wakati jamii ya wanadamu inapokumbatia maovu haya “huja ghadhabu ya Mungu” (Waef 5:5-6, Wakolosai 3:5-6).

Kile kinachojulikana kama kipindi cha dhiki kuu ni nini? Biblia inatuambia ni hukumu tu ya Mungu kwa dunia baada ya kikombe cha uovu wake kujaa (Ufu 16:19). Dunia isidhani itaendelea na maovu yake salama bila kuwajibishwa na Muumba wake. Kile kilichoipindua Sodoma na Gomora sasa kimeenea kila taifa, hivyo kuiweka dunia yote mahali pa hukumu.

Uovu wa wanadamu sasa umeiva sana, naam kama zabibu tayari kwa kukamuliwa (Ufu 14:17-20), na hukumu ya Mungu iko karibu kama mawingu meusi ya mvua yanavyokaribia kudondosha maji juu ya uso wa nchi. Kinasubiriwa kitu kimoja tu mambo yalipuke, nacho ni unyakuo wa kanisa.

Enyi walimwengu yafahamuni haya; mtakaposikia watu wametoweka kila mahali, msijisumbue kuwatafuta, tunawaambia mapema, watakuwa wamenyakuliwa kwenda kwa Baba yao ili kupisha ghadhabu kuu ya Mungu iwanyeshee mliokataa kumpokea yeye aliye pekee Mwokozi wa watu na dhambi zao-Kristo Yesu. Heri afuaye mavazi yake wakati huu maana dunia haina tena wakati wa kusubiri, mzigo wake umeilemea mno. Yesu anarudi. Maranatha!