Uwezo wa Kuchagua na Kuamua

Moja ya zawadi kubwa Mungu aliyotupa wanadamu ni uwezo wa kuchagua na kuamua tutakacho. Hali hii hututofautisha na wanyama ambao hufanya yale wafanyayo kwa kuitikia silika (instincts) walizonazo tu. Hawawezi kufikiri na kuchagua kuamua mambo ili labda wapate maendeleo fulani. Ndio maana wote hufanana katika kile wafanyacho na hawaendelei kimaisha. Lakini mwanadamu ni tofauti. Yeye ana akili, na utashi unaomwezesha kuchagua na kuamua atakalo kulifanya kwa faida yake na wengine. Tofauti na mnyama, yeye anao uwezo wa kubadilisha mazingira yake.

 

Zawadi hii ama kwa hakika imemweka mwanadamu katika tabaka la juu zaidi kuliko viumbe wengine waliomo humu duniani. Lakini pamoja na hadhi hiyo, pia imamfanya awe kiumbe mwenye kuwajibika na maamuzi yake. Nisemacho hapa ni kwamba Muumba wake atamwajibisha kwa kila uamuzi afanyao. Kila uchaguzi na uamuzi una matokeo yake. Na kwa kuwa mwenye kufanya maamuzi hayo hufanya kwa hiari yake basi anawajibika pia kwa matokeo yanayofuata. Hii ndiyo sababu ya msingi Mungu atamhukumu mwanadamu.

 

Ni muhimu sana kufahamu kwamba hakuna uamuzi tuufanyao tukiwa na akili timamu usiohusisha matumizi ya uwezo wetu wa kuchagua na kuamua. Hatuwezi kukwepa kuwajibika na yale tuamuayo kwa sababu yoyote ile. Kwamba ni kukasirika, kuendea taamaa za macho au za mwili, kutokumtii Mungu katika maagizo yake au chochote kingine. Hasira au kuwa na kinyongo au chuki na mtu kwa mfano ni uamuzi tu.

 

Inawezekana mtu akamfanyia mwenzake mabaya sana hivyo akashawishika kumchukia. Lakini bado ukweli unabaki kwamba vishawishi havimlazimishi mtu kuchukua hatua yoyote. Vyenyewe kama vinavyoitwa humshawishi tu mtu, humvuta na kumsukuma kufanya jambo. Lakini mtu akikataa kukubaliana na mvuto au msukumo huo hakuna kitakachotokea. Kumbe basi hatimaye mtu huyu humchukia mwenzake kwa sababu ya kuchagua tu.

 

Alichofanya shetani kule bustanini Eden ni kumshawishi Hawa kufanya uamuzi kinyume na Neno la Mungu. Lakini hakumlazimisha, hata leo adui huyu hutumia miilli yetu, mazingira yetu, na wanadamu wenzetu kutudanganya ili tuchague na kuamua yasiyofaa akijua tutawajibika na matokeo yake.

 

Ni mara ngapi umesikia Neno la Mungu pengine likikuonya umpe Yesu maisha akuokoe lakini unapata mawazo ya kuahirisha kuokoka kwa sababu ya vishawishi au kuwaogopa watu? Ni mara ngapi umeonywa ujiandae Yesu anarudi upesi, utengeneze maisha yako kwa kutubu dhambi na kuuonyosha mwenendo wako? Au ni mara ngapi wewe mtu uliyeokoka umesikia mahubiri na mafundisho yakikuasa udumishe utakatifu wa kweli na kumtumikia Mungu kwa kadiri ya vipawa alivyokupa lakini huchukui hatua? unadhani uamuzi wako wa kutokumtii Mungu hautakuwa na matokeo? Hima mwendee Yesu ukatengeneza mambo yako haraka kwa sababu uvumilivu wa Mungu una mwisho na siku ya kuvuna unayopanda inakuja mbio!

Rev. E. S. Munisi