Unajitambulishaje kwa Ulimwengu?

 

Utambulisho ni kitu muhimu sana. Watu huhusiana na wenzao na kuwatendea kulingana na wanavyowatambua. Kama wakikutambua kama mtu mwenye staha, mwadilifu, mwema na mambo kama hayo watakuheshimu. Wakikuona au hata kukudhania tu kama mtu mwongo, tapeli, watakudharau na kuepukana na wewe. Kumbe basi namna unavyojitambulisha kwa watu ni muhimu mno.

 

 

Siku moja askari wa usalama barabarani (Traffic Police) mkoani Arusha akiwa kwenye opereshini maalum alimkamata dereva mmoja akaanza kumpa amri; “washa indiketa ya kushoto,” “washa ya kulia,” “shika breki,” nk. Vyote alivyoamuru vilidhihirisha kuwa gari ilikuwa bovu. Askari akawa mkali, akaanza kumfokea dereva. Lakini mwenyewe kwa utulivu mkubwa akajibu akamwambia; “ndio naipeleka gari garage,” na mara akaanza kuondoa gari. Askari kuona hivyo akakasirika zaidi, akaona kwamba dereva amemdharau, akafungua mlango wa gari wa mbele ulioko pembeni mwa dereva kwa nguvu akaingia na kukaa.

 

Yule dereva akamwangalia akamwuliza kama kwa kumkebehi; “unataka nikupe lifti au?” Askari kukasirika zaidi sana, akazidi kufoka huku dereva ametulia bila papara yoyote. Wakati pukurushani hiyo ikiendelea askari wengine kadhaa wa usalama waliokuwepo eneo hilo wakawa wanalisogelea taratibu hilo gari. Mmoja wao ambaye alikuwa mkubwa wa wenzake alipomwona yule dereva mara alikakamaa na kupiga saluti huku askari aliyemkamata akiwa pembeni anashangaa. Kumbe aliyekamatwa alikuwa afisa wa JWTZ wa ngazi ya juu sana.

 

Yule askari mara alimtaka radhi na kushuka haraka kwenye gari hilo. Muda mfupi tu alikuwa akimchachafya dereva huyo lakini alipomtambua tu akamtetemekea na kumtaka radhi kwa jambo ambalo wala halikuwa kosa. Hiyo tofauti ilitokana na nini? Utambulisho tu.

 

Hii kweli katika ulimwengu wa roho kama ilivyo kwenye huu wa mwili pia. Biblia inatuambia kwamba mara kwa mara nguvu za giza, yaani mapepo, yalipokutana na Yesu walimtambua ni nani na walimheshimu na kutii alipowaamuru kuwatoka watu (Marko 3:11). Ndivyo walivyowatendea pia waamini walipotumwa na Kriso (Luka 10:17-19), na hata kwenye kitabu cha matendo ya Mitume. Itakumbukwa kwamba wale wana wa Skewa walijaribu kutoa pepo kama walivyomwona Paulo akifanya, lakini pepo aliwajibu akisema; “Yesu namjua, na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani…?” (Mdo 19:15)

 

Kumbe basi ni muhimu sana mtu wa Mungu ujitambulishe ipasavyo. Hii ina maana kwamba ni lazima kwanza ujitambue wewe mwenyewe ni nani mbele za Mungu na uishi hiyo, bila kujionea haya. Ni muhimu ujikubali kama akuitavyo Mungu. Kujitambulisha sio kwa maneno matupu tu, bali kwa kuishi maisha yanayofanana na utambulisho huo. Neno linakutambulisha kama mwana wa Mungu, mtakatifu, mbarikiwa, mshindi na zaidi ya mshindi. Basi wewe usijinene kama mwenye mikosi, dhaifu, mwenye laana, maana huo sio utambulisho wako. Ila ukiung’ang’ania utakuwa wako na shetani na watu watakuelewa hivyo na kukutendea hivyo.

 

Basi ingia kwenye Neno, jikubali kama lenyewe likunenavyo. Jitambulishe hivyo mbele za shetani na kazi zake kwa kinywa na kawa tendo. Tambua aliye ndani yako ni mkuu kuliko aliye katika dunia. Vaa sare ya askari wa Yesu na vyeo vyako wazi wazi mabegani mwako, nawe utashuhudia shetani na kazi zake wakipiga saluti mbele yako kwa utukufu wa Mungu.

 

 

 Author : Rev. E. S. Munisi