Dk. Besigye na hatari ya kuwa rafiki wa Rais mtarajiwa - Kampala, Uganda

  • UN yataka aachiwe haraka
  • Polisi wasema ni mhaini hatari

Kuna usemi mashuhuri usemao, “Tenda wema uende zako ukingonja shukrani yatakufika makubwa”! Naam pengine swahiba wa zamani wa Rais Yoweri Kaguta Museven, Dk. Kizza Besigye, aliudharau usemi huo, lakini sasa anaukumbuka akiwa nyuma ya nondo za gereza lenye ulinzi mkali na hatima ya kesho yake ikitegemea hekima ya majaji na shinikizo kutoka nje.

Mpiganaji huyu wa msituni, aliyewahi kuishi Tanzania akiwa nyuma ya Museven miaka ya nyuma wakati wakipigana kuiangusha serikali ya Uganda ili kuunda mfumo wa kidemokrasia, aliwahi kuliambia shirika la Utangazaji la Uingereza kuwa alimwamini “rafiki” yake Rais Museven kuliko hata alivyomuamini baba yake mzazi. Wakati wote wakiwa porini aliishikilia vyema bastola yake kwa ajili ya kumlinda kuliko alivyojilinda yeye mwenyewe, lakini hali haikuwa hivyo wakati wanafiki walipoingilia kati na urafiki wao.

Kulingana na Taarifa ya Shirika la Utangazaji la BBC, Dk. Besigye licha ya kuwa mpiganaji wa msituni pamoja na Rais Museven yuko Gerezani chini ya ulinzi mkali akisubiri kusikilizwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili baada ya kujiapisha mwenyewe eti kuwa rais wa mioyo ya waganda mara baada ya kutangazwa kushidwa katika uchaguzi wa hivi karibuni.

Kiongozi huyo aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani nchini Uganda cha FDC, amewasilisha jalada kwenye mahakama kuu ya jiji la Kampala, akiomba kupatiwa dhamana, licha ya kuwa anakabiliwa na shitaka la Uhaini ambalo kwa kawaida halina dhamana na akipatikana na hatia hukumu yake ni kunyongwa au kufungwa maisha gerezani. Besigye ambaye kwenye maombi yake alitumia anuani ya gereza la Luzira kama makazi yake, aliandika sababu 10 ambazo mawakili wake wanadhani kuwa zitaishawishi mahakama ikubali kumuachia kwa dhamana, ikiwemo kufikisha umri wa miaka 60 na kutoingilia upelelezi unaoendelea dhidi yake.

Haya yanajiri wakati ambapo mahakama kuu iliukatalia upande wa mashitaka kuhamisha kesi ya Besigye kutoka jijini Kampala. Uamuzi wa Besigye kuomba kupatiwa dhamana umekuja baada ya majuma kadhaa ya kushuhudia kesi yake ikiahirishwa mahakamani kwa kile upande wa mashitaka unachodai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Ofisi ya mwendesha mashitaka nchini Uganda wameiambia mahakama kuwa, Besigye hana vigezo vya kupewa dhamana kutokana na kosa lenyewe. pamoja na uwezekano wa yeye akiwa nje kuingilia upelelezi unaoendelea. Vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Uganda, vinakosoa mfumo wa mahakama kuingiliwa na mamlaka za Serikali, ambapo wanadai kuwa maamuzi yanayotolewa na majaji kwenye kesi hiyo, yamekuwa ya kuegemea upande wa Serikali. Mara kadhaa wabunge wa upinzani wamekuwa wakishinikiza Serikali kumuachia huru Besigye, ambapo wakati wa usomwaji wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, wabunge hao waliingia na mabango na kupiga kelele kumtaka Rais Museveni amuachie huru rafiki yake kwa kuwa mashitaka dhidi yake ni unafiki wa kisiasa na mnyororo wa kusalitiana baina ya marafiki wanaopigana hadi kuingia Ikulu.

Watafiti wa historia wanaeleza kuwa kumekuwa na matukio mengi ya watu wanaowasindikiza marafiki zao kuingia ikulu kuishia ama gerezani, kufukuzwa au kupata “ajali za kisiasa” lakini mwisho wa siku wanatengwa na wale waliowasaidia kuingia Ikulu.

Pengine Dk. Besigye ndiye amekuwa mfano au ushahidi wa madai haya kwani alikuwa mpiganaji pamoja na Museven katika harakati za ukombozi wa Uganda na alipoingia madarakani akasalia kuwa daktari wake anayeonja chakula Rais anachokula. Kwa kadiri siku zilivyoenda ikadaiwa kuwa ameandika waraka wa kupinga mpango wa siri wa Rais Museven wa kumpandisha vyeo mwanaye jeshini ili baadaye kuitwaa Ikulu. Mambo yalipozidi Besigye alitimkia ughaibuni, lakini alirejea na kuanzisha chama cha kisiasa kilichoshiriki uchaguzi na yeye mwenyewe akiwa mgombea. Hata hivyo kile Ikulu ya Kampala ilichopinga kukifanya, yaani njama za kumpandisha mwana wa Rais vyeo, kimetimia kwani karibuni amerushwa vyeo vitatu huku mke wa Rais akichaguliwa kuwa Waziri wa Elimu.

Wakati msuguano ukiendelea Umoja wa Mataifa umeitaka Uganda kumuachia kiongozi huyo wa kisiasa mara moja, lakini ombi hilo limepokelewa kwa mtazamo hasi na waendesha mashitaka wakidai kuwa suala hilo ni la ndani halihitaji amri ya nje.