UFUNUO WA YOHANA

Price:Tsh. 12,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:Ijapokuwa kitabu hiki cha Ufunuo kimejulikana kama “Ufunuo wa Yohana,” chenyewe kinajitambulisha kama “Ufunuo wa Yesu Kristo.”Kinaanza na neno la faraja, “Ufunuo” sio “Mafuniko.” Ni faraja iliyoje kuona kitabu hiki kikimtumainisha msomaji kwamba ujumbe wake sio ujumbe uliofunikwa bali umefunuliwa ili kila asomaye auelewe!

Wengi wamekata tamaa wasomapo kitabu hiki na kuona humo lugha ya mafumbo, wakadhani ni kitabu kilichofungwa, kisichoweza kueleweka. Lakini neno la kwanza kabisa la kitabu ni “ufunuo,” na narudia: SIO MAFUNIKO. Kwa hiyo kinaweza kabisa kueleweka kwa kuwa kimekusudiwa hivyo na mwenye kukitoa, yaani Mungu. Yohana anaandika:

Ufu 1:1-3

1Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa Malaika amwonyeshe mtumwa wake Yohana, 2aliyelishuhudia Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani mambo yote aliyoyaona. 3Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.

Maana ya Neno “Ufunuo”

Neno “Ufunuo” limetafsiriwa kutoka kwenye neno la Kiyunani “Apokalupsis” lenye maana ya kufunua kilichokuwa kimefunikwa au kusitirika, kuweka wazi yale ambayo kabla hayakuwa yanafahamika. Sio neno geni, wala halikuanza kutumika hapa kwenye kitabu cha Ufunuo. Limetumika sehemu zingine mbalimbali za Biblia kama Luka 2:32, Wagal 1:12, 2Wathes 1:7, 1Pet 1:7)

Hii ni kusema kwamba katika ujumbe wa kitabu hiki Mungu anaweka wazi mambo ambayo hapo kabla hayakuwahi kujulikana kwa uwazi kiasi hicho. Ni kwa nini Mungu ametaka kuweka wazi ujumbe sasa? Kitabu chenyewe kinatupa sababuwakati wa utimizo wake umekaribia.

Ufunuo huu unaitwa “…wa Yesu Kristo.” Hii ina maana mbili: maana ya kwanza ni kwamba ufunuo huu unatoka kwa Yesu Kristo; yeye ndiye asili yake. Maana yake ni kwamba huu sio ujumbe wa kibinadamu, bali ni wa kiungu kwa kuwa umetoka moja kwa moja kwa Mungu. Maana ya pili ni kwamba ujumbe huu unamfunua Kristo. Yaani huu ni ufunuo wa Yesu Kristo kama alivyo. Maana hii nayo ni pana sana kwenye kitabu hiki.

Yesu Kristo Akiwa amefunuliwa kwa Sifa zake Mbalimbali

Kuhani Mkuu, Bwana, Mchungaji

Katika sura ya kwanza Yesu anafunuliwa akiwa katika uhusiano wa karibu na kanisa lake duniani. Tunamwona Yesu aliyetukuzwa anavyohusiana na kanisa duniani kama Kuhani wake mkuu, Bwana wake, Mchungaji wake mwema, Mhukumu wake, Nguvu, na Kimbilio lake.

Simba wa Kabila la Yuda, Mwana-kondoo Aliyeshinda, Jaji wa Dunia

Katika sura ya tano, anafunuliwa kama Mwana Kondoo aliyeshinda, “Simba aliye wa kabila la Yuda shina la Daudi” mwenye mamlaka ya kuihukumu na kuipiga dunia kama Jaji wake mkuu. Na sura zinazofuata, yaani sura ya sita hadi ya kumi na tisa, anaonekana akitekeleza vilivyo mamlaka yake kuu ya kuihukumu na kuipiga dunia katika kipindi chote cha dhiki kuu.

Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana

Kwenya sura ya kumi na tisa, anafunuliwa sio kama Jaji wa dunia tu, bali pia kama Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana. Anadhihirishwa akija duniani kutoka ikulu ya mbinguni huku akisindikizwa na msafara wa mabilioni ya askari wa kifalme ambao ni Malaika, na Mawaziri wa serikali yake mpya yaani kanisa litakalokuwa lilikwisha kunyakuliwa kabla, pamoja na nguvu na utukufu mwingi, akiwa amekwisha kutunukiwa ufalme wa dunia atakaoumiliki kwa miaka elfu moja, na baadaye milele na milele kwenye mbingu mpya na nchi mpya.

Bwana wa Vita, Hodari wa Kuokoa

Katika ujio huo wa kifalme, anafunuliwa kama Bwana wa vita, na “hodari wa kuokoa” hapo anapoonekana akiwaokoa watu wake Israeli katika vita hivyo vya Harmagedon, huku akiwashinda kabisa-kabisa adui zake watakaokuwa wakiongozwa na mpinga Kristo, katika vita ya wazi inayoshuhudiwa ya ulimwengu, na mbingu kwa pamoja.

Jaji wa Walio Hai na Wafu, Mhitimishaji wa Historia

Kwenye sura ya ishirini anafunuliwa kama Jaji wa wanadamu wote, na Mhitimishaji wa historia ya ulimwengu. Hili analifanya hapo anapoonekana akiwa ameketi kwenye kiti kikubwa cheupe akiwahukumu wanadamu wa vizazi vyote katika historia ya dunia. Mazingira ya hukumu hiyo yanatisha sio kwa wanadamu tu, bali pia hata mbingu (anga) na nchi zinaonekana zikiukimbia uso wake, huku kuzimu yenyewe ikiwatoa wafu wake ili watokee mbele ya Jaji wao kwa hukumu ya mwisho.

Imanueli wa Milele kwa Walio Wake

Kwenye sura ya ishirini na moja na ishirini na mbili anafunuliwa kama Mungu aliye pamoja na watu wake kwa uhusiano wa karibu kwenye mbingu mpya na nchi mpyaImanuel wa Milele. Anaonekana akiwa amemkabidhi Mungu Baba enzi yake, naye Baba akiwa yote katika yote. Kama alivyokuwa stadi wa kazi katika uumbaji kwenye kitabu cha Mwanzo, anaonekana kama mhitimishaji wa uumbaji wote wa asili, na Mkuu katika ulimwengu mpya wa utukufu. Ama kweli ndiye Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, Mwenyezi.

Kiini cha Ujumbe wa Ufunuo

Kitabu kinataja mapema kiiini, yaani neno lake kuu, kuwa ni “….mambo ambayo kwamba hayana budi kuwepo upesi.” Ni mambo gani haya ambayo yanatarajiwa kutukia upesi? Kitabu chenyewe kinayanena mbeleni kwamba ni matukio siku za mwisho yatakayolipata kanisa kwa upande mmoja, na dunia kwa upande mwingine.

Protokali ya Kiungu kwenye Ufunuo Huu

Yohana anasema ujumbe huu Mungu (akiwa na maana ya Baba) alimpa Yesu Kristo ili awaoneshe watumwa wake. Naye Yesu akamtuma Malaika amwonyeshe Yohana. Lakini anayetawala simulizi hii, na kuusema Ujumbe huu ni Roho Mtakatifu. Hii inaonekana katika sura ya pili na ya tatu hapa isemwapo mara kwa mara; “…Yeye aliye na sikio na alisikie Neno hili ambalo Roho ayaambia Makanisa….” (2:7, 11, 17, 29, 3:6, 13, 22).

Hii inatuonesha ni jinsi gani Uungu wote unavyohusika na kitabu cha Ufunuo. Kwa utaratibu wa kiprotokali Baba anamkabidhi Mwana Ufunuo huu, naye kwa Roho Mtakatifu anaunena kwa Kanisa kwa utumishi wa Malaika aliyemwonesha Mtume Yohana, naye Yohana analikabidhi kanisa kitabu cha ujumbe huo.

KUSOMA UJUMBE MZIMA PATA NAKALA YA KITABU HIKI