UAMSHO NA UREJESHO

Price:Tsh. 8,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:


MIAMKO SITA ILIYOTIKISA DUNIA (1727-1906)

Sio lengo langu kuangazia historia nzima ya Ukristo tangu mwanzo wa kanisa pale Yerusalemu katika makala hizi. Hilo tunaliacha akiba kwa wakati mwingine. Nimechagua vipindi hivi vinavyojulikana katika historia ya kanisa kama “Miamko Mikuu Sita” (The Great Six Awakenings) kwa kuwa katika hivi mtu anaweza kuona:

  • Jinsi uamsho mmoja ulivyozaa mwingine mkubwa zaidi.
  • Mambo yaliyokuwa kwenye kila uamsho ambayo ndiyo ushahidi na alama za uamsho wa kweli.
  • Mambo ya kujihadhari nayo, yaliyo hatari katika wakati wa uamsho.

Mwamko (Uamsho) wa Kwanza

Huu ni uamsho ulioanzishwa na kikundi cha Wa-Moravian wachache kilichokuwa kikijulikana kama Herrn hut au Mkesha wa Bwana mnamo mwaka 1727. Kiongozi wa uamsho huu alikuwa ni Nikolas Count Ludwig Von Zinzendorf, Mjerumani. Uamsho huu ulianza kama mkesha wa masaa 24 wa maombi, mkesha ambao ulidumu kufanyika kwa miaka 100 baadaye.

Miaka 65 baada ya kuanza uamsho huu, hiki kikundi kidogo cha waombaji kilikuwa kimetuma Wamisionari 300. Moto wa uamsho huu ulirukia Uingereza na hatimaye Marekani ukizaa watumishi wa Injili ambao nao waliwasha moto mkubwa uliosambaa nchi mbalimbali. Uamsho huu uliliwasha kanisa la Anglikana la Uingereza, Presbyterian la Scotland, Baptist la Pennsylvania, Virginia, na Massachusetts Marekani. Katika kipindi cha miaka 20 makanisa mapya 150 yalizaliwa, na kati ya 1740-1742 peke yake watu wapatao 30,000 waliokoka na kujiunga na kanisa.

Uamsho huu pia, uliwaandaa wanauamsho maarufu, George Whitefield na John Wesley, walioasisi uamsho wa karne ya 18 wa ki-injili (Evangelical). Wawili hawa walitokana na uamsho huu wa kwanza. George Whitefield alikuwa anahubiri mikutano ya watu hadi 30,000 kwa wakati mmoja, maelfu ya hao wakiwa wanaokoka katika karibu kila mji wa Uingereza, Scotland, na Wales. Alivuka bahari ya Atlantic mara saba, na kuhubiri miji ya Boston, New York, na Philadelphia ya Marekani ambamo wengi waliokoka. Idadi ya jumbe alizohubiri hadharani zilizohesabiwa ni 18,000.

John Wesley, aliasisi kanisa la Methodist, alisafiri juu ya mgongo wa farasi maili 250,000 akihubiri Injili (jumbe 40,000 jumla), aliandika vitabu 233. Alipofariki aliacha watumishi nyuma yake, aliokuwa amewaandaa kwa huduma 750 Uingereza, 350 Marekani. Kanisa alilolianzisha la Methodist aliliacha likiwa na washirika 76, 968 Uingereza, na 57,621 Marekani. Akishirikiana na nduguye Charles, alitunga nyimbo za Injili 9000 (elfu tisa). Mengi ya mafundisho yake yalisababisha kuzaliwa, na yanafundishwa na Wa-Holiness, Wana-Uamsho, Wa-Pentekoste, na makundi ya Karismatik hadi leo.

Uamsho wa Pili

Uamsho huu nao ulianza kama uamsho wa maombi mnamo mwaka 1784. Hii ilikuwa ni baada ya John Erskine wa Edinburgh kuchapa upya kitabu alichokuwa ameandika Jonathan Edward, kiitwacho, An Humble Attempt to Promote Explicit Agreement and Visible Union of God's People in Extraordinary Prayer for the Revival of Religion and the Advancement of Christ's Kingdom (Jaribio la Unyenyekevu la Makubaliano Mahsusi na Umoja ulio dhahiri wa Watu wa Mungu Juu ya Maombi Yasiyo ya Kawaida kwa ajili ya Uamsho wa Kidini na Kuendeleza Ufalme wa Kristo).

Mwiitikio ulikuwa mkubwa sana kwa watu waliosoma kitabu hiki. Dhehebu moja baada ya jingine lilijitolea kuomba na kufunga kila Jumatatu moja ya Mwezi. Hayo yalifanyika kwanza Uingereza, kisha Marekani nayo ikafuatia. Katika kipindi hicho mmomonyoko wa maadili ulikuwa mkubwa kufuatia vita vya uhuru Marekani, mapinduzi ya Ufaransa, maanguko ya kiroho kwa wengi katika makanisa ya Ulaya, jambo lililosababisha wenye macho ya kiroho kuona hitaji kubwa la kumtafuta Bwana upya kwa ajili ya uamsho. Matokeo ya maombi haya yalianza kuonekana kwa kuzaliwa uamsho huu wa pili kwenye miji ya Yorkshire mwishoni mwa mwaka 1791, ukaenea kila mahali na kila Dhehebu lililokuwa limeupokea ujumbe wa kitabu cha Edward.

Ukuaji wa kanisa ulikuwa wa kushtusha: Kanisa la Methodist lilikua idadi ya washirika kutoka 76,968 hadi 250,000, Makanisa ya Wales yakajaa tena, na viwanja vya wazi vikawa vinajaa watu wanaofika kusikia Injili. Kutokana na uamsho huu, taasisi mbalimbali za Injili zilianzishwa, zikiwemo, British and Foreign Bible Society, The Religious Tract Society, The Baptist Missionary Society, The London Missionary Society, The Church Missionary Society na nyingine nyingi.

Mguso wa uamsho huu kwa jamii ya dunia ulikuwa mkubwa sana pia. Mfano kanisa la Kiinjili la Ki- Anglikana wakati huo lilipokea uamsho na matengenezo ambayo yalilifanya lipambane vikali na biashara ya utumwa na hatimaye kufaulu kutokomeza kabisa biashara hiyo haramu, hali za magereza zilirekebishwa, na taasisi mbalimbali za maafa zikaanzishwa. Marekani makanisa yalipokea mwamko mkubwa wa maombi, na wimbi la kuokoka vijana wa shule na vyuo vikuu. Wimbi hili lilidumu hadi mwanzoni mwa miaka ya 1820.

SURA YA PILI

VIPINDI SITA VYA UAMSHO ULIOIGUSA DUNIA-2

Vipindi vilivyofuata kama vinavyoonekana hapa chini vinakumbukwa kipekee kwa sababu ya ukuu na kudumu kwa mguso wake kwa ulimwengu. Historia inaonesha kuwa wahusika wa vipindi hivi waliacha hazina kubwa katika maisha na mjengo wa mafundisho kwenye maisha ya kanisa dunisani isiyoweza kusahauliwa.

Uamsho wa Tatu

Kijiti cha mbio za uamsho wa pili kilipokelewa na Charles Finney pamoja na wenzake Asahel Nettleton wote wa Marekani. Katika uamsho wa Charles Finney idadi ya watu 100,000 waliokoka katika kipindi cha mwaka mmoja tu, bila kuhesabu wengine waliookoka baadaye katika mikutano yake. Mikutano ya Injili ya Finney ilitikisa miji kwa kiwango cha kustaajabisha. Viwanda, maduka, na baa zilifungwa ili watu wahudhurie mikutano yake. Kwenye miji mingine baa zilifungwa moja kwa moja kwa kuwa hakukuwa na mtu alikunywa pombe, kwani mji mzima uliokoka!

Uweza wa Bwana ulikuwa mkuu sana katika mikutano ya Finney kiasi kwamba nyakati nyingine wasiookoka walikuwa wanaanguka kutoka kwenye viti vyao kama waliokufa bila kuguswa na mtu, na wakiinuka wanatoka kumpokea Bwana. Huduma ya Finney iliambatana na maombi mazito yake mwenyewe na mwombaji mwingine aliyejulikana kama Father Nash. Finney alizoea kuomba kuanzia saa kumi alfajiri hadi saa nne asubuhi. Sio tu kwamba idadi kubwa ya watu waliokoka kwenye mikutano yake, bali pia wengi wao waliendelea na Wokovu. Inasemekana kuwa 80% ya watu waliokuwa wanakata shauri kuokoka waliendelea kudumu na Wokovu.

Uamsho wa Nne

Uamsho huu ulianza Canada 1857. Waalimu wengine wa historia ya kanisa, kwa kuuona uamsho wa Finney kuwa sehemu ya ule wa pili, wanauita huu wa Canada kuwa ndio wa tatu. Huu ulikuwa ndio uamsho ulioenea eneo kubwa zaidi ki-jiografia, na kuwa na mguso mkubwa kuliko Miamko mingine iliyokuwa imetangulia.

Mwanzo wake ulikuwa wa taratibu sana ambapo watu 21 tu walianza kuokoka, kisha ikawa watu kati ya 25 na 40 huokoka kila siku. Hatimaye makanisa ya Marekani yakaanza kushika moto wa uamsho. Mnamo mwezi Septemba, mwaka 1857 mfanya biashara mmoja, jina lake Jeremiah Lanphier, aliyekuwa ameokoka miaka kumi kabla katika mikutano ya Finney, alianzisha maombi ya kila Jumatano mchana katika mji wa New York. Mwezi uliofuata Octoba, hiki kikundi kidogo cha maombi kiliamua kukutana kila siku badala ya Jumatano pekee. Uamsho huu wa maombi ya wafanyabiashara ulienea haraka. Ndani ya miezi sita tu idadi ya watu wapatao elfu kumi walikuwa wanaomba sehemu mbalimbali nchini Marekani.

Mungu aliitikia kwa nguvu maombi ya washirika hawa. Kati ya mwezi Februari na Juni 1858, watu wapatao 50,000 walikuwa wakiongezeka kanisani kila wiki! Mwaka 1865 uamsho huu ulishaota mbawa na kuiramba Uingereza, na kusababisha watu 500,000 kuokoka. Huko Ulster watu 100,000 waliokoka, Scotland watu 30,000 waliokoka, na Wales watu 100,000 waliokoka.

Kama kawaida ya uamsho wa kweli uzaavyo watumishi hodari, na kubadilisha jamii inayoizunguka, uamsho huu nao uliwatengeneza watumishi kama, D. L. Moody na Sankey, William na Catherine Booth, Walter na Phoebe Palmer, Charles Haddon Spurgeon, Hudson Taylor aliyeanzisha China Inland Mission, Gawin Kirkham aliyeanzisha Open Air Mission. Yule Mmisionari maarufu David Livingstone aliyefia Africa ni zao la uamsho huu ulioanza na maombi ya wafanyabiashara wachache huko New York ukaenea Dunia nzima. Kukua kwa haraka sana kuliripotiwa barani Ulaya, Urusi ya magharibi, Australia, South Seas, Africa ya Kusini, na India.

Uamsho wa Tano

Kati ya mwaka 1882-1903, dunia ilishuhudia uamsho mwingine wa tano. Dwight L. Moody, aliyekuwa ameandaliwa na uamsho uliotangulia, alikuwa mstari wa mbeli kati ya wenzake, akiukimbiza mwenge wa uamsho mpya. Uamsho huu wa tano ulizaa huduma kubwa zenye upako wenye makali yaliyo dhahiri, uinjilisti wa D. L. Moody ulistawi sana.

Moody aliaza huduma yake huko Chicago Marekani, alifanya mikutano mikubwa ya injili iliyotajwa kuwa na mafanikio makubwa sana. Inaaminika kuwa yeye alikuwa ameitwa na Bwana achukue cheche za uamsho uliotangulia na kuuwasha moto wa uamsho mpya Dunia nzima. Alisafiri na mwimbaji wa Injili Ira Sankey, kwenye mikutano yake huko Uingereza, Ireland, na Scotland ambamo kumbi kubwa za miji hiyo zilikuwa zikijaa watu waliokuwa wakihudhuria mikutano yake. Huduma aliyoifanya huko Cambridge 1882, iliasisi huduma ya Wordwide Interdenominational Student Missionary Movement. Ijapokuwa YMCA, na Jumuiya za Kikristo (Christian Unions) zilikuwa zimeshaanzishwa kutokana na uamsho uliotangulia, ni Moody ndiye aliyezibadilisha kuwa huduma zenye nguvu na za ki-Misheni.

Miongoni mwa vijana walioguswa sana na uamsho huu ni vijana wa kimarekani ambao walijitolea kwenye kazi za kimisheni. Msukumo huu wa ari ya utumishi kwa vijana katika uamsho wa D. L. Moody uliwafanya vijana hawa kuandaliwa kuwa viongozi mahiri wa uamsho mkubwa uliofuata wa karne ya 20. Chuo alichokianzisha Moody cha Moody Bible Institute, mwaka 1883, kilikuwa na mchango mkubwa sana katika juhudi za kimisheni. Shirikisho la kikristo la kimisheni lilianzishwa wakati huu na A. B. Simpson. Kile kijulikanacho kama Christian Endeavor Movement ilianzishwa huko Portland. Wainjilisti wengi kama Sam Jones, J. Wilber Chapman na Billy Sunday walipokea moto wa uamsho kwa Moody.

Huko Africa ya kusini Andrew Murray alikuwa na mafanikio makubwa katika huduma. Mambo yalikuwa hivyo hivyo huko Australia, huko Japan idadi ya washirika iliongezeka kutoka 4000 hadi kufikia 30,000 katika kipindi cha miaka mitano. Ni katika kipindi hiki makanisa yalifunguliwa kwa wingi ulimwenguni na hivyo kuweka tayari mazingira kwa ajili ya uamsho uliofuata wa karne ya ishirini.

Uamsho wa Sita

Uamsho uliofuata wa sita ndio ule ulio maarufu zaidi kama Uamsho wa Wales. Ulianza mnamo septemba 22 1904, na Evan Robert akiwa mkimbizaji mwenge wake. Itakumbukwa kwamba, huu uamsho wa Wales uliungana kwa haraka na ule wa Azusa miaka miwili tu baada ya kuanza kwake, yaani 1906. Ulipozaliwa uamsho wa Wales, ulienea kwa kasi ulaya nzima. Watu walipokea Roho Mtakatifu, uponyaji, na kama kawaida ya uamsho wa kweli, wengi wakaokoka. Taarifa hizi zilipofika masikioni mwa Wamarekani ambao tayari walikuwa na njaa kubwa ya kiroho kwa sababu ya Holiness Movement, ziliwaandaa vizuri sana kiroho kuupokea Uamsho mkubwa uliokuwa ufuate mara.