MISINGI YA KUUKULIA WOKOVU

Price:Tsh. 6,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:


Siku za leo, tofauti na ilivyokuwa miaka thelathini iliyopita. Neno “wokovu” au “kuokoka” sio neno geni masikioni mwa wengi. Hata nyimbo za “waliookoka,” siku hizi zinavuma kutoka kijijini hadi kwenye makusanyiko makubwa mijini kama vile; kwenye arusi, mikutano ya injili, vituo vya mabasi na hata kwenye mikutano ya kisiasa.

Tofauti na miongo mitatu iliyopita, siku hizi watu waliookoka wapo kwenye makundi yote ya jamii. Wapo wakulima vijijini, wafanyakazi na wafanyabiashara mijini, wasomi wa vyuo vikuu, wanasiasa na viongozi wa serikali, viongozi wa mashirika, makampuni, majeshi yote na kila aina ya makundi ya watu.

Kwa ajili ya hayo, inaweza kunenwa leo ya kwamba, kwa sehemu, ujumbe wa wokovu umeenea na kusambaa kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miongo mitatu iliyopita. Kanisa limejieneza kwa mapana na marefu. Yaani limesambaa kijiografia, na katika makundi ya kijamii kuanzia yale ya chini kiuchumi na kielimu hadi yale ya juu kabisa nchini.

Lakini liko tatizo moja kubwa sana katika ukuaji huu au kusambaa huku kwa kijiografia kwa kanisa. Tatizo hili ni kwamba, katika ukuaji wake, kanisa halikuzingatia kukua kwa kina. Limekazana na kukua kwa mapana na marefu tu, yaani kujieneza kijiografia, kiidadi na kwa makundi ya kijamii tu, huku likisahau kwa sehemu kubwa sana kama sio kabisa, kukua kiroho katika maarifa ya Neno la Mungu.

Huku kukua kiroho katika maarifa ndiko ninakokuita kukua kwa kina, yaani kumjua Mungu kwa undani.

Kanisa la Afrika linanenwa ulimwenguni siku hizi kuwa ni kanisa lililokua kijiografia na kiidadi kwa maelfu ya maili, lakini kwa kina lina sentimeta moja tu! Yaani ni kanisa kubwa kwa idadi ya waamini na limeenea kwa maelfu ya maili, lakini kwa ukuaji wa maarifa ya Mungu, kina chake cha ufahamu ni kama sentimeta moja tu. Hii ni hatari kubwa!

Yapo makanisa mengi leo yana ukuaji usio wa asili (unnatural growth). Huku ni kukua kiidadi kwa haraka, kusikozingatia malezi ya kiroho, kujenga nidhamu ya kiroho na kuwafanya waamini kuwa wanafunzi wa kweli wa Yesu kama lilivyo agizo kuu la Bwana Yesu, (Math. 28:19-20).

Ni kama walivyo wale kuku wa kisasa, wanaokuzwa ndani ya wiki tatu na kuuzwa tayari kwa kuchinjwa na kuliwa! Kusema kweli hawa bado ni vifaranga, sio kuku. Ukuaji wao sio wa asili, yaani sio wa kawaida ya maumbile, ni wa kulazimisha. Unapokula kuku hawa ujue unakula vifaranga tu, ijapokuwa wanaonekana kwa umbo ni wakubwa, na madhara yao kiafya ni makubwa.

Makanisa mengi leo yana waamini wengi ambao kwa kweli ni “vifaranga,” hawajawa “kuku” bado. Wengine katika hawa wanaodhaniwa kuwa ni “kuku” wamepewa (na wengine wamejipa) majukumu makubwa ya kihuduma—majukumu yawapasayo watu wazima kiroho, (1Tim 3:1,6).

Kwa sababu hiyo kazi ya Mungu imeingia hatarini kwa sababu “vifaranga” hawa kwa kukosa malezi, wengi wao wanafundisha na kufanya yaliyo mapotofu.

Siku za leo sio ajabu kumwona mtu ameokoka Januari, na Septemba ukamsikia akitangaza kuwa eti yeye ni Mtume na Nabii, Askofu Mkuu wa Kanisa lake, na “specialist” mwenye “Upako” wa kuponya magonjwa sugu, yaliyoshindikana kuponywa kwa maombi ya watumishi wote! Ingeishia hapo tusingeshtuka sana, lakini baya zaidi ni yale yanayosikika yakitoka vinywani mwa “watumishi” hawa. Yaani mafundisho yao potofu, na jinsi watoto wa Mungu walio wachanga wanavyopotoshwa nayo. Kanisa ni jengo, kama lisipokuwa na misingi mirefu na kujengwa vyema, wakati linaendelea kujengwa kwenda juu, litafika mahali litashindwa kuhimili uzito wake wenyewe na kuanguka.

Katika siku hizi za mwisho, tunapofanya bidii kuivuna mioyo ya Watanzania kwa Yesu, hatuna budi kukumbuka kuwa, UVUVI WA MIOYO NI LAZIMA UENDE SAMBAMBA NA MALEZI YA WAONGOFU WAPYA, BILA KUSAHAU NA WALE WA ZAMANI, ili Kanisa likue, sio kwa mapana na marefu tu bali pia kwa kina. Vinginevyo tutajikuta “tunazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, tunamfanya mwana wa jehanum mara mbili kuliko alivyokuwa mwanzo, (Math. 23:15).” Hilo Mungu, apishe mbali.

Ni rahisi kwa ajili ya shauku ya kukuza kanisa kiidadi na kijiografia, kutia bidii zaidi katika juhudi za kuleta watu kwa Yesu na kusahau kule kuwafanya waliokwisha kuokoka kuwa wanafunzi wa Yesu. Hii ni kwa sababu, kuwafanya waamini kuwa wanafunzi, kunadai gharama kubwa ya kila namna; bidii ya kuandaa na kufundisha masomo yanayotakiwa, muda, pesa, nidhamu kuu ya kiroho na nguvu kazi watu.

Lakini ni muhimu tukumbuke kuwa, ukuaji wa kweli wa ki-Biblia wa Kanisa ni ule tu unaowaelekeza waamini mara baada ya kuokoka, “KUDUMU KATIKA FUNDISHO LA MITUME, na katika USHIRIKA, na katika KUUMEGA MKATE, na katika KUSALI” (Mdo. 2:41-41).

Kitabu cha Matendo ya Mitume, kinauonesha kwa wazi sana ukweli huu. Kila mahali Mitume walipoanza Kanisa, kulifuatiwa na juhudi kubwa sana ya mafundisho ya mfululizo maalumu (systematic teaching).

Kama nilivyosema, Kanisa ni jengo, lina msingi, nguzo, kuta nk; linajengwa hatua kwa hatua, jiwe juu ya jiwe, na hatimaye wajenzi wake watapokea thawabu kwa mwenye nyumba (1Wakor. 3:9-15).

Huu ni ujenzi wa fundisho juu ya fundisho. Kuanzia mafundisho yanayolenga kumwekea mwamini misingi mirefu na imara katika Bwana tangu siku anapookoka (Waebr. 6:1-2) hadi, mafundisho yanayomfanya “kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo,” (Waef. 4:13).

Kitabu hiki kimekusudiwa kumsaidia mwanafunzi wa darasa la waongofu wapya, aliyeokoka katika kipindi cha mwaka mmoja kupata misingi muhimu ya mafundisho itakayomuimarisha katika maisha yake ya kiroho. Kimeandikwa kimfae pia Mwalimu ili afundishe kwa mtiririko unaotakiwa. Kimegawanyika katika sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza nimeiita “JITAMBUE.” Sehemu hii inamzungumzia mwamini na kilichomtokea, mwamini na Neno la Mungu, mwamini na mazingira yake-ufahamu wake, mwili wake, dunia, na shetani, na Ahadi ya Baba.

Lengo la sehemu hii ni kumuimarisha mwamini kwa kumpatia zana muhimu zitakazomwezesha kushinda majaribu yake ya awali kama mtoto mchanga na kumsaidia kuanza vyema safari yake ya maisha ya ushindi kiroho, inamsaidia kujiona kama Mungu amwonavyo. Katika sehemu hii, mwanafunzi anapaswa afundishwe tangu siku ile ya kwanza au ya pili ya kuokoka kwake, ni muhimu sana.

Haipasi mtu anayeokoka asubiri mpaka wiki ipite (hata kama anaokoka kwenye mkutano wa Injili), ndipo aanze kupata mafundisho ya awali.

Mtoto anapozaliwa huanza kunyonya pale pale, akisubiri aje anyonye wiki moja baadaye, atakuwa ameshakufa. Hii ni moja ya sababu mikutano mingi ya Injili, huandaliwa hata kwa gharama kubwa sana na wanaokoka watu wengi sana lakini hawaendelei na imani baada ya mkutano.

Wanakufa njaa na kwa kushambuliwa na mbwa-mwitu kabla hata mkutano haujaisha, huku wazazi wao wa kiroho wakiwa wanasherehekea mkutano, wakijibariki kulia na kushoto, wakijiimbia, “mbariki aliye kushoto kwako, na kulia kwako …bariki, amen, bariki amen,” wasijue kuwa wakati wao wanajibarikia na kwenda zao nyumbani kulala, adui shetani anafanya kazi mchana na usiku kushindana na lile Neno lililopandwa mioyoni mwa wale waliookoka ili awarudishe nyuma, (Math. 13:18-23).

Sio vibaya kujibarikia, lakini ni uzembe wa kiroho kuishia kujibarikia na kusherehekea mkutano huku tukiwa tumewasahau watoto wanaozaliwa mkutanoni hapo na kuwaacha wafe njaa.

Ni vyema semina ya waongofu wapya ifanyike kipindi kile kile mkutano unapoendelea, na kila anayeokoka awe na mlezi wa kumlea kwa karibu kila siku katika siku zake za awali tangu pale anapokata shauri kuokoka. Shetani hasubiri mkutano uishe ndipo aanze kuwashawishi waliookoka kurudi nyuma, huanza pale pale wanapookoka.

Kanisa amka, uwalee watoto wa Mungu wanaozaliwa mikononi mwako, kwani utatoa hesabu kwa ajili ya watoto hao mbele za Baba yao!

Ule usemi “kuzaa sio kazi, kazi ni kulea” ni wa kweli hata kwenye malezi ya watoto wa kiroho pia. Ni lazima tukubali kulipa gharama ya malezi. Tusimalize mkutano au kumshuhudia mtu kisha tukarudi kulala, na kudhani tumemaliza kazi, ukweli ni kwamba, kazi ndiyo kwanza imeanza!

Sehemu ya pili ni; “WEWE NA KANISA.” Sehemu hii inalenga kumsimika mwamini katika wajibu wake kwa mwili wa Kristo yaani Kanisa. Inamwongoza kuutambua umuhimu wa kuwa mshirika wa Kanisa la mahali pamoja na kulihudumia Kanisa lake ipasavyo.