Masuala yaliyopo leo Kwenye tafsiri za Unabii

Price:Tsh. 8,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:

WILLIAM MILLER NA UNABII WA SIKU ZA MWISHO

Pengine mfano mzuri zaidi unaoonesha jinsi ambavyo kukisia tarehe ya kuja kwa Kristo kunavyoweza kuwa na matokeo ya hatari kiimani ni mwanzilishi wa imani ya Seventh day adventists—William Miller (Cairns, 1954). George Miller (1782-1849) awali alikuwa mchungaji wa kanisa la Baptist. Yeye hakupata elimu ya theolojia, ila alikuwa msomaji sana wa Biblia.

Katika kusoma kwake vitabu vya Danieli na Ufunuo, alikutana na unabii wa siku za mwisho. Jambo lililomvutia sana ni unabii wa Danieli 8:1-14). Kutokana na maandiko ya unabii huu aliamini kuwa Yesu angerudi tarehe 21 March 1843. alipofundisha huo “ufunuo” wake wengi walimwamini wakapanda juu ya mapaa ya nyumba na juu ya milima wakimngojea Yesu aje awanyakue. (ibid)

Tarehe iliyopangwa ilipopita bila Yesu kurudi wafuasi wa Miller walishuka juu ya mapaa ya nyumba na milimani wakiwa wamechanganyikiwa wasijue kulikoni. Lakini Miller alirejea tena hesabu zake za Dan 8:14 na akawarudia wafuasi wake na kuwaambia alikuwa amekosea hesabu, na kudai kuwa tarehe ya kuja kwa Yesu ingekuwa 22 October, mwaka uliofuata wa 1844. Lakini tarehe ilipofika Yesu hakurudi. Ndipo Miller akafunga Biblia yake na kuacha huduma, huku akilaani fundisho la kuweka tarehe ya kurudi kwa Bwana. (ibid) Miller alikuwa amejenga fundisho lake kwenye mistari ya mistari ya 13-14 isemayo:

Ndipo nikamsikia Mtakatifu mmoja akinena, na Mtakatifu mwingine akamuuliza huyo aliyenena, ‘hayo maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa yataendelea hata lini kukanyagisha patakafifu pa jeshi?’ Akamwambia, “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu, ndipo patakatifu patakapotakaswa”

Yeye alitafsiri maneno “nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu” kuwa ni miaka 2300, na kutakaswa hekalu kuwa ni Bwana angerudi na kutakasa hekalu la Yerusalemu. Alipohesabu miaka 2300 akianzia pale Ezra aliporudi Yerusalemu mwaka 457 k.k, aliona miaka 2300 ingeishia mwaka 1843, na baadaye akaona ingeishia 1844. (Tutaangalia maana ya unabii wa Dan 8 na maana ya “nyakati za jioni na asubuhi 2300) tutakapotafakari hoja hiyo kama tulivyosema kwenye utangulizi wetu).

Kufuatia kutokurudi kwa Yesu tarehe ambayo Miller alitabiri, wafuasi wa Miller (Millerites, kama walivyojulikana kabla ya kuitwa Seventh Day Adventists), walitaniwa kwenye magezeti na kusumbuliwa makanisani kwa ajili ya misimamo yao jambo lililopelekea kujitenga na kuunda dini yao mpya waliyoipa jina la Seventh Day Adventist mnamo mwaka 1860. (ibid) Baadaye mfuasi wa Miller, Hiram Edson, alifafanua kutokurudi kwa Yesu 1843 na 1844 kuwa ni kwa sababu hekalu lililotabiriwa kuwa angelilitakasa sio la kidunia bali ni la mbinguni, akimaanisha kuwa Yesu aliingingia patakatifu mbinguni na kufanya upatanisho kwa damu yake mwaka 1844. (ibid) Sio tu kwamba tafsiri hii iliuimarisha upotofu wa fundisho la Miller, ila pia ulizaa upotofu mpya na wa hatari zaidi unaoukana ukamilifu wa dhabihu ya Kristo uliokamilika kwa kufa na kufufuka kwake.

Kiongozi wa pili aliyefuata baada ya Miller, Mrs Ellen G. White aliyedai kuona maono ya mbinguni, aliimarisha upotofu wa Miller na Edson, na kuweka msingi mpya wa mkazo wa siku ya sabato kama msingi muhimu wa imani. Kitabu cha Ellen, cha The Great Controversy ni moja ya mihimili mikuu ya imani hiyo (Wright, 1999).