Kuibuka Kwa Imani Potofu

Price:Tsh. 8,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:


MWITO WA KUILINDA IMANI

Mtumishi wa Bwana Yesu, Yuda, alianza kitabu chake kwa maneno ya kushtua akili za kila mwenye kufikiri. Ni kama mtu apigaye mbiu akiwaonya watu juu ya hatari kubwa inayowakabili. Anasema:

Yuda 1:3

3Wapenzi nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwiishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. 4 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye pekee Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.

Picha anayotuonesha Roho Mtakatifu kwa onyo kali hili ni ya watu wenye kitu cha thamani mkononi mwao, kinachowindwa na adui zao huku wenyewe wakiwa hawana habari wala kuchukua tahadhari yoyote. Limekuwa jambo la kawaida kwa watu wa Mungu kujisahau na kuishi maisha ya kufurahia tu wokovu wao bila kuchukua tahadhari ipasavyo kuilinda imani ya wokovu huo. Hii ni kwa sababu watakatifu hawa hawajui kuwa imani waliyo nayo huwindwa sana ili iibiwe na kuharibiwa na adui wao mkubwa-shetani.

Kwa wengi shetani ni kama dhana tu, yaani mtu wa kufikirika badala ya kiumbe halisi, mwenye akili, na mipango kamili kinyume na ufalme wa Mungu. Ni kwa sababu hiyo Yuda, kwa kalamu iliyovuviwa analionya kanisa la vizazi vyote, liamke, akitoa mwito wa kuilinda hii “imani… ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo…” (1Pet 1:7).

Yuda anatalitahadharisha kanisa likumbuke kuwa sio wote wanaoonekana kuwa pamoja nao ni wenzao kweli. Wengine wamejiingiza kwa siri, wakiwa na ajenda zao. Wanaishi kama virusi kwenye kanisa ili hatimaye waliharibu kanisa la Mungu. Lakini ashukuriwe Mungu, “antivirus” ya Roho Mtakatifu ni kali, hataruhusu uharibifu huu utokee kama kanisa likishirikiana naye ipasavyo.

Katika kipindi cha miongo miwili na nusu hivi iliyopita, hapa Africa kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana ya hali ya kanisa. Haya ni mabadiliko ya kukua. Pamoja na ukuaji mkubwa sana wa kanisa kiidadi na hata kwa kusambaa kwake, pia kumeibuka wimbi kubwa sana la imani potofu. Kwa mara ya kwanza tangu wimbi la kipentekoste lilifikilie hili bara wakati huu kumekuwepo haja ya uteteaji wa ndani (Polemics) kwa kiwango kikubwa kuliko wakati mwingine wowote. Kile lilicholitokea kanisa la America miaka ya hamsini, yaani kanisa kupata changamoto ya upotofu mkubwa wa ndani, sasa inaonekana ndicho kinacholitokea kanisa la Africa.

Hapa kwetu Tanzania kasi ya kukua kwa wimbi la imani potofu ni kubwa na madhara yake yameaza kuonekana. Misingi ya kibiblia sasa kwa wengi imekuwa kama msamiati wa lugha ya kigeni. Watoto wa Mungu wanaozaliwa upya, wanajikuta katika mazingira ya hatari. Wanawaona wenzao, kaka na dada zao katika imani, wakikimbia huku na huku, toka kanisa moja hadi lingine, toka kwa huduma moja hadi nyingine. Wakiuliza kulikoni wanaambiwa, “tunatafuta mtumishi mwenye upako zaidi atuondolee shida zetu, magonjwa yetu, na umaskini wetu.”

Isingekuwa shida kama wafikapo kwa hao wanaowaita “watumishi wenye upako” wangekutana na mafundisho yenye uzima. Lakini cha kusikitisha ni kile kinachowatoka baadhi ya hao “watumishi.” Sio tu kwamba wanalisha watu takataka nyingi za kiroho, ila wanawalisha zile taka zenye sumu. Watoto wa Mungu hawa, hawawi tu katika hatari ya utapiamlo wa kiroho, bali kwa kweli wanakuwa katika hatari ya kufa kabisa kiroho.

Na kwa kuwa wengine wanakuwa wameanza na upotofu huo tangu kuokoka kwao inakuwa vigumu mno kwao kuona kama wamepotoka kwa kuwa hawajui aina nyingine ya malezi wala chakula cha kiroho. Kwao muujiza ukitokea ni uthibitisho wa kutosha kuwa na kila lisemwalo kwenye mahubiri ya mtumishi husika ni kweli. Kwa kiwango kikubwa sana wamekuwa kama vifaranga wa tai walioanguliwa na kuku na kujikuta wako katikati ya vifaranga vya kuku. Itawachukua muda kufahamu kuwa wao sio kuku bali tai.

Wengine wamefika hata mahali pa kutafuta watumishi wa “kuwasafishia nyota,” au “kuwaondolea nuksi, balaa na mikosi,” au kuwafungua na “roho ya kukataliwa,” au “kuwavunjia laana.” Siku hizi imekuwa vigumu kutofautisha kati ya mtu anayekwenda kwa Mtumishi wa Mungu na anayekwenda kwa mganga wa kienyeji, kwa sababu yale yale watafutayo kwa waganga wa kienyeji, huyatafuta kwa baadhi ya hawa “watumishi” ambao na wenyewe hujitangaza kama wenye “upako” wa kufanya hayo! Ni jambo la kutisha mtumishi wa Mungu kufanya mambo ya kiganga yaliyotajwa hapo juu.

Siku hizi kuna watumishi ambao hawajali wanafanya huduma kwa namna gani, ali mradi wanapata wafuasi. Sio hivyo tu tumefikia hata mahali tunashuhudia watumishi wengine wakiuza huduma kama kuuza karanga. Mara mwenye shilingi million moja ataombewa maombi maalum, na mwenye shilingi elfu moja atapata maombi ya jumla. Na haya yanafanyika wazi bila haya. Haya yote yanafanyika bila hawa kondoo wasio na hatia kushtuka na kufahamu kuwa wanashughulika na watumishi wa tumbo badala ya watumishi wa kweli wa Mungu.

Hayo tuliyoyataja hapo juu, ni dalili moja tu ya upotofu mkubwa zaidi uliopo nchini mwetu. Ni moshi juu vilele vya miti mirefu msituni unaoshiria moto mkali chini. Yapo mambo makubwa zaidi tutakayoyajadili katika kitabu hiki yanayoonesha mahali tulipofikia, na hatari kubwa inayolikabili kanisa la Tanzania kwa sababu ya kutokufahamu kunakotisha kwa kanisa juu ya uwepo wa hatari yenyewe.

KUSOMA UJUMBE MZIMA PATA NAKALA YA KITABU HIKI