Jinsi ya Kurejesha Vyote

Price:Tsh. 8,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:BADO MUNGU ANAJIBU MAOMBI

Unapoona hupati majibu ya maombi yako usifanye kosa la kujitengenezea sababu za kubuni za kutokujibiwa maombi yako. Eti Mungu hanipendi, au amenisahau, au anataka kunifundisha jambo. Rejea kwenye Neno, nawe utaona likupasalo kufanya daima.

Mungu ni Mungu wa kanuni, hutenda kazi kwa kuzingatia kanuni au njia zake. Kuzifahamu njia zake ni utajiri mkuu sana. Mtu anayefanikiwa katika maisha yake ya maombi ni yule ashirikianaye na Mungu kwa mujibu wa njia zake Mungu Mwenyewe.

Tofauti ya mtu amwonaye Mungu kwa wingi katika maisha yake na yule mwenye ukame wa kiroho asiyemwona Mungu maishani mwake ni moja kubwa: Mmoja anazijua njia za Mungu na hufanya mambo kulingana nazo, mwingine hujua tu kazi za Bwana, anasikia nguvu za Mungu kwa wengine, lakini hajui Mungu hufanya kazi kwa misingi gani, au kwa njia gani. Hii ndiyo iliyokuwa tofauti kubwa kati ya Musa na waisraeli walio wengi. Biblia inabainisha:

Zab 103:7

Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.

Huku kujua njia za Mungu hakukuja hivi hivi tu, Musa mwenyewe alikuwa ametamani na kumwomba sana Mungu amjulishe njia zake. Tunapoanza kuutafakari ujumbe huu, hebu ungana na Musa kumwomba Mungu:

Kut 33: 13

Basi sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbela zako, nionyeshe njia zako, nipate kukujua….

Siku hizi kuna mkazo mkubwa sana wa watu kufanyiwa maombi na watumishi wa Mungu kwa ajili ya matatizo yao mbalimbali. Hili ijapokuwa ni jambo jema kwa upande mmoja, lina hatari kubwa kwa upande wa pili kama tusipokuwa waangalifu. Hatari hii iko katika kuwajenga watu kwa watumishi zaidi badala ya kuwajenga kwenye Neno.

Siko kinyume hata kidogo na kuwafanyia maombi watu, mimi mwenyewe nafanya hayo. Ila huduma hiyo inatakiwa kuambatana na kuwajenga watu kwenye Neno la Mungu na kuwaelekeza kuitumia imani yao kwa Mungu na Neno hilo badala ya kuwafanya waone kama sisi tunaowaombea ndio pekee tunaosikiwa na Mungu, na hivyo kuwafanya getemezi badala ya mashujaa wa imani.

Kipindi hiki cha wimbi la imani potofu tumeshuhudia watu wengi wa Mungu wakiyumba na kuondoa macho yao kwenye Neno na kuyaweka kwa watumishi zaidi, hiyo isingekuwa mbaya kama wangewaona kama watumishi ambao kwao wao wanapokea Neno na huduma ya ule upako uliowekwa juu yao pekee. Biblia inatuambia:

1Wakor 3:5-8

5Basi Apolo ni nani, na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini, na kila mtu kama Bwana alivyompa. 6Mimi nalipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. 7Hivyo apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. 8Basi yeye apandaye na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. 9Maana sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu

Fungu hili la maandiko linaonesha kwamba kazi ya wahubiri na waalimu ni kuwalisha watu Neno ili liwajenge na kuzaa matunda maishani mwao. Yale yanayotarajiwa kuonekana maishani mwa waamini ni matokeo ya wao kuwa watendaji wa Neno.

Lakini tatizo la wengi leo linakuja hapo ambapo badala ya waamini kuijenga imani yao kwenye Neno wao huwaona watumishi kama “ma-star” na wenye majibu yao bila wao wenyewe kushiriki katika kuijenga imani yao wapate kupokea wenyewe kwa Mungu wao. Ama wanasahau au hawajui kwamba wahubiri ni wapanzi wa “mbegu” ya Neno la Mungu na wao ni “shamba la Mungu.” Na kwa msingi huo ni juu ya shamba kupokea na kuzaa mazao yatokanayo na Mbegu zinazooteshwa humo.

KUPATA UJUMBE MZIMA, PATA NAKALA YA KITABU HIKI