Jinsi ya Kufundisha Neno Kwa Ufanisi

Price:Tsh. 6,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:
Simon Petro ni miongoni mwa wanafunzi wa Bwana Yesu waliokuwa maarufu sana kati ya wale thenashara. Umaarufu wake ulitokana na mambo mengi. Hakuna jambo au tukio lenye utukufu wa pekee kipindi chote cha huduma ya Yesu duniani ambalo haonekani kushiriki. Lakini moja kati ya hilo ambalo bila shaka hakuweza kusahau ni maneno Bwana aliyomuusia baada ya kufufuka kwake muda mfupi tu kabla ya kupaa kwake mbinguni, kama anavyoandika mtume Yohana (Yoh 21:15-19).

Mara tatu mfululizo Bwana alimuuliza Petro swali, “Je, Simon wa Yohana wewe wanipenda kuliko hawa?” Naye akamjibu, “Naam Bwana wewe wajua kuwa nakupenda” naye Bwana akamwambia, “Lisha wana kondoo wangu.” Haya yaliporudia mara tatu Petro alihuzunika. Kwa kurudia swali lile lile mara tatu alikuwa kama anagonga neno hilo moyoni mwa Petro kama kugongea msumari, mpaka lilipoingia ndani sana hata likawa sehemu ya utu wake. Alikuwa anamwambia Petro kuwa namna atakayoweza kumwonesha kuwa kweli anampenda ni kwa kuwalisha kondoo wake. Hii ni kwa kuwa kondoo wake ni wa thamani sana kwake. Anakumbuka kuwa amewanunua kwa damu yake mwenyewe (Mdo 20:28).

Watumishi wote katika kanisa, kwamba ni washirika wa kawaida au kwamba ni wale waliotengwa kwa kazi ya Injili, wote walifundishao Neno la Bwana kwa watu wake na wakumbuke kuwa wanafanya kazi ya moyoni mwake Kristo—kuwalisha wana kondoo wake. Na anadai tuifanye kazi hiyo kutoka kwenye ule moyo wa kumpenda kwa dhati. Ni mapenzi hayo pekee, ndiyo yatatutia nguvu na himizo kukubali kujinidhamu katika kazi hii inayodai moyo, akili, muda, fedha, na hata wakati mwingine uhai wetu kuifanikisha. Kulisha kondoo wa Bwana sio kitu cha kufanya kama fadhili kwa Bwana, ni wajibu wa msingi, ni KAZI, na moja ya kipimo cha upendo wetu kwake.

Haiwezekani kuifanya kazi hii kwa ufanisi kama tusipoelewa na kukubali kuwa ni jukumu kubwa lisilowezekana kufanywa kivivu wala kwa moyo wa kusitasita. Lakini pia ni kazi yenye thawabu kubwa mbele za Bwana. Ujumbe wa kitabu hiki unawapa changamoto watumishi wa lile Neno kukukumbuka kuwa ufanisi wa kazi hii unategemea umakini, bidii, na maisha yaliyotolewa kwa Bwana asilimia mia moja.

Watumishi, kufundisha ni upishi. Hakuna mpishi aliyefaulu kwenye kazi yake asiyetoa muda wake mwingi kuandaa chakula. Kupika kunahitaji muda na umahiri mkubwa. Na hii ni kazi, tena kazi kubwa. Sio jambo la kulipua-lipua. Kitabu hiki kinakukumbusha kwamba KUFUNDISHA KWA UFANISI NI KAZI, na ni lengo linalofikika, lakini linahitaji kuamua, kujitolea, na kuipenda kazi yenyewe. Na siku moja tutasimama mbele ya mwenye kondoo hawa na kupokea ile “taji ya utukufu, ile isiyokauka” (1Pet 5:4), jipe moyo Mchungaji, na Mwalimu, kwa kuwa unayemtumikia ni mfalme hodari mwenye haki, sio dhalimu hata aisahau taabu yako katika utumishi huu.

KUSOMA UJUMBE WOTE PATA NAKALA YA KITABU HIKI