Dondoo Za Unabii za Siku za Mwisho

Price:Tsh. 8,000


Author: Rev. E. S. Munisi


Publisher / Printer : NIIM COMPUTERS


Dar es Salaam, Tanzania


Edition:


Ufunguo wa Kuelewa Unabii wa Siku za Mwisho

Imenenwa na wengi kwamba Biblia ni msitu mkubwa sana, na mtu akitembea humo anaweza kupotea njia. Wasemao haya humaanisha kwamba ni vigumu kuielewa Biblia. Kwa sehemu usemi huu ni kweli. Kama mtu asipopata mwongozo wa kuelewa somo lolote analotaka kujifunza katika kitabu hiki cha kipekee hawezi kulielewa. Towashi aliyekuwa anasoma chuo cha nabii Isaya aliulizwa na Filipo, “…je, yamekuelea haya unayosoma?” (Mdo 8:30) Naye akamjibu, “…nitawezaje kuelewa mtu asiponiongoza?” (Mdo 8:31) Kila somo katika Biblia lina ufunguo wa kulielewa. Hata vitabu vinavyounda Biblia, kila kimoja ujumbe wake unaweza kueleweka kikamilifu pale tu mtu anapofahamu kiini au neno kuu la kitabu husika.

Unabii wa simu za mwisho ni moja ya mosomo muhimu sana ya Biblia. Kama yalivyo masomo mengine, hili nalo lina ufunguo wake ambao mtu asipokuwa nao hawezi kulielewa. Hapa tuna maana kuwa somo hilo muhimu lina neno kuu au kiini chake na shabaha yake inayolipa uelekeo, ambayo kuielewa hiyo humpa mwanafunzi mwanga wa kuuelewa unabii na siku za mwisho kirahisi, kwa mapana, na kwa kina ipasavyo vikiwepo vitabu vya Danieli na Ufunuo wa Yohana. Ufunguo huo ni UFALME WA MUNGU. Hili ndilo neno kuu la somo la Unabii wa siku za mwisho na Injili kwa ujumla. Injili ya Bwana Yesu inajulikana kama “habari njema ya ufalme.” (Math 4:23, 9:35, 13:19) Biblia inaunena ujumbe aliohubiri Yesu kwa maneno haya:

Marko 1:14-15

14 Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani Yesu akaenda Galilaya akihubiri habari njema ya Mungu, 15 akisema WAKATI UMETIMIA NA UFALME WA MUNGU umekaribia tubuni na kuiamini injili.

Maneno haya “wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia” yamepewa mkazo katika fungu la maandiko haya kwa kusudi la kuonesha msisitizo wa neno kuu yaani somo kuu katika unabii wa Biblia; amblo ni wakati wa ufalme wa Mungu kuja ulimwenguni. Kwa maneno mengine kuna kusudio la kiungu kuondosha aina zote za ufalme au utawala duniani wakati uliokusudiwa na kuusimika ufalme wa kiungu (theokrasia) duniani, ambapo Mungu mwenyewe atawatawala wanadamu moja kwa moja. Andiko hilo hapo juu lilikuwa mwito wa Mungu kwa watu wake Israeli kujiandaa kiroho kwa kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa umekaribia. Na Katika kitabu cha Ufunuo 1:5-6 tunakutana tena na maneno haya:

5Tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, 6na KUTUFANYA KUWA UFALME, NA MAKUHANI kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Maneno “na kutufanya kuwa ufalme na makuhani” yanadhihirisha kuwa kuna ufalme, yaani utawala ambao Mungu anauandaa kwa ajili ya watoto wake. Hawa ni watatawala pamoja na Mfalme Yesu, ambaye Biblia imemuelezea kama kaka yao mkubwa kwenye ufalme huo. (War 8:29) Tuangaie fungu lingine hapa chini huku macho yetu yakiwa yanatafuta kwa makini maneno yauhusuyo ufalme huu, na jinsi yanavyohusishwa na siku za mwisho.

Ufunuo 11:15 -17

15 Malaika wa saba akapiga Baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, UFALME WA DUNIA UMEKWISHA KUWA UFALME WA BWANA WETU NA WA KRISTO WAKE, naye atamiliki hata milele na milele. 16 Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu 17 wakisema, Tunashukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako uliomkuu, na kumiliki. Hapa kuna maneno ya ajabu kidogo, yanayohitaji kuangaliwa kwa makini. Maneno yasemayo “Ufalme wa Mungu umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake,” yanadhihirisha kuwa katika kalenda ya Mungu kumekuwepo na kipindi kirefu ambacho Mbingu zimekuwa zikisubiri wakati ambao ufalme wa dunia utakuwa chini ya mikono ya Mungu na Kristo Mwana wa Mungu. Maana yake hii ni nini? Kwani Mungu hatawali dunia yote kama mfalme wake?

Wakati tunatafakari hili pengine tuongeze na swali hili: Kwa nini Yesu alipowafundisha wanafunzi wake ile iitwayo “sala ya Bwana” aliwafundisha kuomba “ufalme wako Uje…?” (Math 6:9) Huku ufalme wa Mungu kuja hapa duniani kutoka mbinguni kuna maana gani kinabii? Na Je, andiko tulilolinukuu hapo juu hapo Malaika wanapoonekana wakishangilia na kusema “ufalme wa dunia umekwishakuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake,” linatimiza matarajio ya kinabii yanayodhihirishwa na hii sala ya Bwana? Naam, kama tutakavyoona punde kidogo, hivo hasa ndivyo ilivyo kwamba linatimiza matajio ya kinabii na lengo kuu la unabii wote katika Biblia.

Ufalme wa Mungu ndio kiini na lengo kuu la unabii wote katika Biblia. Yesu aliye somo kuu la Biblia ametabiriwa kuwa Mfalme atakayetawala dunia hii, kwa kipindi maalum, na hatimaye milele na milele kwenye mbingu mpya na nchi mpya. Kuuelewa ufalme wake na mchakato wa kuujenga ufalme huo ndio siri, na ufunguo wa kuelewa na kutafsiri ipasavyo unabii wa siku za mwisho.

KUSOMA UJUMBE MZIMA PATA NAKALA YA KITABU HIKI